Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fiji yachukua hatua kuwa na boti itumiayo nishati isiyozalisha kabisa hewa ya ukaa

Vijana wafanyao kazi kwenye boti hiyo Uto ni Yalo wakiandaa kung'oa nanga kwenye mji mkuu Suva nchini Fiji ili kusambaza vifaa vya misaada kufuatia kimbunga kilichopiga nchi hiyo mwaka 2018
Uto ni Yalo Trust/Samuela Ulacake
Vijana wafanyao kazi kwenye boti hiyo Uto ni Yalo wakiandaa kung'oa nanga kwenye mji mkuu Suva nchini Fiji ili kusambaza vifaa vya misaada kufuatia kimbunga kilichopiga nchi hiyo mwaka 2018

Fiji yachukua hatua kuwa na boti itumiayo nishati isiyozalisha kabisa hewa ya ukaa

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshuhudia hatua dhahiri za taifa la Fiji za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanakumba nchi hiyo na nyingine zilizoko kwenye bahari ya Pasifiki bila ya wao kuwa wachangiaji wa uharibifu wa mazingira.
 

Hatua alizoshuhudia ni pamoja na boti ambayo haisababisha kabisa uchafuzi wa mazingira, boti iliyopatiwa jina ‘Uto ni Yalo’ ambayo alipata fursa ya kuipanda na kusafiri nayo kwenye bahari hiyo ya Pasifiki.

Boti hiyo Uto ni Yalo imejengwa kwa kutumia stadi za asili pamoja na vifaa vya kisasa na teknolojia za kisasa ambapo stadi hizo za kiasili zinahamishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Mathalani Guterres ameona paneli za sola ambazo zinatumika kwa ajili ya kupatia nishati boti hyo.
Uto ni Yalo, imesafiri mara mbili duniani katika umbali wa maili 80,000 za baharini ikitembelea mataifa yaliyo kaskazini na kusini mwa dunia ili kuhamasisha ahadi kutoka kwa jamii, wafanyabiashara na watunga sera za kulinda visiwa na bahari.

Ravesi Waqanibaravi, ni mmoja wa wafanyakazi kwenye boti hiyo ambapo ikiwa safarini amemweleza Katibu Mkuu ya kwamba, “tunajaribu kutumia stadi za kijadi kwa kadri tuwezavyo. Hii ni boti isiyotoa kabisa hewa chafuzi, na hii ni kuonyesha kwamba inawezekana kurejesha usafiri wa baharini ulio endelevu.”

Kisha boti hilo lilitia nanga na Katibu Mkuu alitembelea eneo la kurejeleza taka kwenye Chuo Kikuu cha South Pacific na kushuhudia jinsi wanafunzi vijana wanachukua hatua ili kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Wanafunzi hao wanachukua chupa cha plastiki na kuzichakata katika vipande vidogo ili kutengeneza bidhaa nyingine ambapo mwanafunzi Kathan Nambiar amesema, “unachukua tu chupa ya plastiki, au aina yoyote ile ya plastiki na unaiweka hapa na inachakatwa kuwa vipande vidogo vidogo pindi unapotumia mashine kuichakata na kisha tutatumia mashine nyingine kuumba kitu tunachotaka.”

Katibu Mkuu amehitimisha ziara yake ya siku mbili Fiji na kesho atakuwa Tuvalu, taifa lingine la visiwa lililoko kwenye bahari ya Pasifiki.