Guterres aendelea kupigia chepuo hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Guterres aendelea kupigia chepuo hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani huko nchi za visiwa vya Pasifiki, leo amehutubia mkutano wa jukwaa la viongozi wa visiwa vya ukanda huo akiangazia mambo makuu mawili ambayo ni changamoto siyo tu kwa eneo hilo bali ulimwengu mzima kwa ujumla.
Akihutubia mkutano huo kwenye mij mkuu wa Fiji, Suva, Bwana Guterres ametaja changamoto hizo kuwa ni ongezeko la madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi na tishio linaloongezeka dhidi ya bahari duniani.
Katibu Mkuu amesema vichocheo vya mabadiliko ya tabianchi viko dhahiri akitaja ongezeko la utoaji wa hewa chafuzi ambayo amesema umefikiwa viwango vya juu zaidi kuwahi kufikiwa na hakuna dalili za kupungua.
“Miaka minne iliyopita ilikuwa na joto kupindukika. Kutoweka kwa theluji huko Greenland ncha ya kaskazini mwa dunia kunazidi kushika kasi, ikimaanisha kuwa viwango vya maji ya bahari vitaongezeka kwa mita moja ifikapo mwaka 2100 iwapo hakuna hatua zinachukuliwa kudhibiti,” amesema Katibu Mkuu.
Amesema kwa upande wa bahari ya Pasifiki, ongezeko la kiwango cha maji ya bahari katika maeneo mengine ni mara nne zaidi kuliko kiwango cha wastani duniani na hivyo kutishia uwepo baadhi ya nchi za visiwa.
Ametaja madhara mengine yatokanayo na majanga ya asili kama vile vimbunga, milipuko ya volcano na matetemeko ya ardhi kuwa ni viashiria vya jinsi nchi hizo za visiwani huko ukanda wa Pasifiki ziko hatarini, “na mabadiliko ya tabianchi yatazidisha zaidi hizi hatari ambazo zinaathiri pia afya ya umma.”

Katibu Mkuu amesema mabadiliko ya tabianchi nayo yanatishia usalama akinukuu azimio la Boe lililoridhiwa mwaka jana.
Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema tayari ameunda jopo la kubainisha uhusiano dhahiri kati ya mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usalama akisema, “nina hamu ya kuwasikiliza na kushauriniana nanyi zaidi kuhusu suala hili.”
Hata hivyo amepongeza jinsi nchi za visiwa vya Pasifiki zimekuwa zikichukua hatua dhidi ya changamoto za sasa na zijazo zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, “mnaandika historia ya hatua za kukabili mabadiliko na matumizi ya ufahamu wa kiasili. Mnapatia changamoto wale waliozoea hali ilivyo.”
Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umeazimia kusaidia jitihada za mataifa hayo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kubadili mwelekeo ambao unatishia uwepo wa tamaduni zao na visiwa hivyo.
“Ndio maana nimeomba Ufaransa, Jamaica na Qatar ziongoze uhamasishaji wa jamii ya kimataifa ili kupata dola bilioni 100 kwa mwaka kuanzia mwaka 2020 ili kusaidia mataifa yanayoendelea katika kuhimili na kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu.
BAHARI NAZO ZIKO HATARINI
Katibu Mkuu amegusia jinsi ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanaathiri ustawi wa bahari ambayo ni muhimu katika uchumi na utamaduni wa nchi zilizoko kwenye bahari ya Pasifiki.
“Kiwango cha joto baharini kinaongezeka, sambamba na kiwango cha aside na hivyo kusababisha matumbawe kupata rangi nyeupe na kuharibu bayonuai.”Guterres amesema.
Amesema kando mwa ongezeko la joto, shughuli nyingine kama vile uvuvi kupita kiasi nao unatishia rasilimali za baharini huku kiwango cha oksijeni baharini kikipungua na hivyo kusababisha hatari ya kutoweka kwa baadhi ya viumbe vya baharini.
Visababishi vingine ni taka na plastiki zinazotupwa baharini akisema, “kila mwaka tani zaidi ya milioni 8 za plastiki hatari hutupwa baharini. Tafiti za hivi karibuni zaidi zinaonesha kuwa iwapo hakuna hatua zinachukuliwa, kiwango cha taka za plastiki kitazidi kiwango cha samaki baharini ifikapo mwaka 2050.”
MAJIBU TUNAYO: SEPTEMBA NAWAKARIBISHA NEW YORK
Ingawa amepongeza hatua za mataifa mbalimbali ikiwemo ya ukanda wa Pasifiki kukabili hali hiyo, amesema ni vyema kuwe na hatua za kasi zaidi kwa ajili ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa bahari.
“Hii inahitaji hatua zilizo sambamba na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, ajenda 2030 pamoja na mkataba wa kimataifa kuhusu bahari,” amesema Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa mbinu na mifumo ipo cha msingi sasa ni udharura, utashi wa kisiasa na nia ya dhati “na ni kwa msingi huo nitakuwa mwenyeji wa mkutano wa kuchukua hatua kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, utakaofanyika New York, Marekani mwezi Septemba mwaka huu.”
Katibu Mkuu amesema mkutano huo utakuwa fursa kwa mataifa kuongeza ahadi zao ili ziweze kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2020 na hatimaye kutotoa kabisa hewa hizo ifikapo katikati mwa karne ya sasa.