Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atoa wito kwa viongozi kuchukua maamuzi yenye busara kulinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezuru Vanuatu katika hatua ya mwisho ya ziara ya Pasifiki kushuhudia athari za mbadiliko ya tabianchi.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezuru Vanuatu katika hatua ya mwisho ya ziara ya Pasifiki kushuhudia athari za mbadiliko ya tabianchi.

Guterres atoa wito kwa viongozi kuchukua maamuzi yenye busara kulinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amehitimisha ziara yake ya wiki moja katika visiwa vya pasifiki huku akitoa wito kwa viongozi wa dunia kufanya maamuzi yaliyo na busara kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa sababu sayari dunia nzima ipo hatarini. 

Bwana Guterres ameongeza kwamba, katika kipindi cha wiki nzima, ameshuhudia binafsi athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye  mataifa ya visiwa vya pasifiki. Ameongeza kuwa, “yana mchango mdogo sana katika janga la mabadiliko ya tabianchi duniani kote lakini ndio mataifa yanayoathirika kwa kiasi kikubwa.”

Katibu MKuu huyo ametoa angalizo kwamba mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa uhai akitolea mfano vijiji ambavyo vinahamishwa, njia za kujipatia kipato zinaharibiwa na watu wanapata magonjwa yatokanayao na mabadiliko ya tabianchi, na kusisitiza kwamba, “hatari zimo dhahiri.”

Aidha ameongeza kwamba, akiwa nchini Tuvalu alishuhudia taifa nzima likipigana kuhakikisha uwepo wake akisema, “cha kutia matumaini ni kwamba licha ya changamoto kubwa ambazo nchi hizi zinakabiliana nazo lakini zimeamua kwamba hazitakata tamaa, zimeamua kutafuta suluhu na zimeimarisha mbinu za kukabiliana na athari na kujijengea mnepo.”

Halikadhalika bwana Guterres amesema kwamba, “ mataifa hayo yanaongoza katika kupunguza hewa chafuzi na ni mfano ambao mataifa mengine yanapaswa kuiga.”

Katibu Mkuu huyo amekumbusha kwamba vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi sio vita vya mataifa ya visiwa vya pasifiki tu lakini ni vita vya dunia nzima.

Bwana Guterres amerejelea kauli yake kwamba vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi vinahitaji dhamira ya kisiasa kwa ajili ya mabadiliko katika sera kuhusu kawi, usafiri, viwanda na kilimo na ni kwa mantiki hiyo amependekeza mambo manne kwa viongozi wa mataifa ya visiwa vya pasifiki ikiwemo, "mosi kuhamisha kodi kutoka kwenye mishahara na kuihamishia kwenye bidhaa zinazozalisha hewa ukakaa, akisema toza kodi uchafuzi wa mazingira sio watu , Pili kukomesha ruzuku kwa sekta ya mafuta kwani fedha za walipa kodi hazipaswi kuchagiza vimbunga, kusambaza ukame na ongezeko la joto, kuyeyusha theluji na kubabua matumbawe, tatu kuacha  ujenzi mpya wa viwanda vya  makaa ya mawe ifikapo mwaka wa 2020 na nne tunahitaji uchumi unaojali mazingira na sio unaoyasambaratisha.”

Katibu Mkuu huyo amesema kinachohitajika sio ushikamano, au ukarimu ni maamuzi yenye busara kutoka kwa viongozi wote kwa sababu sio tu mataifa ya pasifiki yako hatarini bali ni sayari dunia yote. Na kukwamua pasifiki ni kuikwamua dunia.

Tweet URL