Eneo la Katwa, Kivu Kaskazini, linaongoza kwa visa vya Ebola-WHO

5 Aprili 2019

Shirika la Afya duniani WHO linasema kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa wa Ebola kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC na eneo la Katwa linaongoza kwa maambukizi zaidi. 

Ripoti ya WHO iliyochapishwa katika tovuti ya shirika hilo ikiangazia kipindi cha siku 21 kuanzia tarehe 13 Machi hadi tarehe 2 mwezi huu wa Aprili,  inaonesha vituo vya 57 katika kanda 12 za kiafya vimeripoti visa vipya.

Katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 172 wamethibitishwa kuwa na Ebola na kuripotiwa ambapo Katwa ina wagonjwa 50, Vuhovi wagonjwa 34, Mandima wagonjwa 28, Masereka wagonjwa 18, Beni 13, Butembo 12, Oicha wanane  Kayna watatu, Lubero watatu, huku Kalunguta, Bunia na Musienene kila eneo likiwa na mgonjwa mmoja mmoja.

WHO inasema kwa kushirikiana na wadau wao wataendelea kutumia mikakati na pia kuboresha juhudi zao kuzuia kuenea zaidi kwa Ebola katika maeneo hayo.

Kufikia tarehe Pili mwezi huu,  jumla ya wagonjwa 1100 wamethibitika na kwa mujibu wa WHO, ambapo 633 ni wanawake,  320 ni watoto wenye umri wa chini  ya miaka 18.

Idadi ya wahudumu wa afya walioathirika imepanda kutoka wahudumu 78 hadi 81 yaani asilimia 7 ya visa vyote vikiwemo vifo 27.

Aidha ripoti ya WHO inaeleza kuwa wagonjwa 338 ambao walipokea matibabu katika vituo vya Ebola tayari wameruhusiwa kurejea nyumbani.

Mlipuko wa sasa huko DRC kwenye jimbo la Kivu Kaskazini  ulianza mwezi Agosti mwaka jana baada ya mlipuko mwingine kuripotiwa mapema mwaka jana kwenye jimbo la Ituri.

Wafanyakazi wa WHO kitengo cha kupambana na Ebola wakifika eneo la Komanda, Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, Januari 2019.
WHO/Lindsay Mackenzie
Wafanyakazi wa WHO kitengo cha kupambana na Ebola wakifika eneo la Komanda, Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, Januari 2019.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter