Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vituo viwili vya kutibu Ebola Katwa na Butembo vyafungwa, visa vipya 6 vya Ebola vyaripotiwa

Kituo cha kutibia Ebola katika hospitali moja mjini Beni, mkoa wa kivu Kaskazini DRC
MONUSCO/Alain Coulibaly
Kituo cha kutibia Ebola katika hospitali moja mjini Beni, mkoa wa kivu Kaskazini DRC

Vituo viwili vya kutibu Ebola Katwa na Butembo vyafungwa, visa vipya 6 vya Ebola vyaripotiwa

Afya

Kufuatia matukio ya kutiwa moto kwa kituo cha kutibu Ebola cha Katwa na kile cha Butembo kushambuliwa na watu wenye silaha wasiojulikana, vyote jimboni Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeripotiwa hii leo kuwa vituo hivyo viwili sasa havifanyi kazi kabisa. Shirika la afya ulimwenguni, WHO ambalo limelaani kitendo hicho, sasa linahofu kuwa ugonjwa huo unaweza kusambaa zaidi kutokana na hatua ya baadhi ya mashirika ya kiraia kuondoa wafanyakazi wake kutoka eneo hilo. Martial Papy Mukeba wa Radio  Okapi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO anaripoti zaidi.

Kituo cha kutibu Ebola cha Katwa kilichomwa moto siku tano zilizopita, ilhali kile cha Butembo kilishambuliwa na watu wenye silaha wasiojulikana siku mbili zilizopita kabla ya kufungwa zilizikuwa zinasimamiwa na madaktari wasio na mpaka, MSF na Wizara ya Afya ya DRC.

Kituo pekee cha muda cha kutibu Ebola ambacho kinafanya kazi sasa ni kile kilichopo kwenye hospitali ya Katwa kikiongozwa na ALIMA.

Mashambulizi haya mawili yamechochea MSF na ALIMA kuondoa wafanyakazi wao wa matibabu kutoka Butembo na Katwa. Daktari Michel Yao, kiongozi wa operesheni za dharura katika WHO barani Afrika anatoa tahadhari juu ya hatari ya kusambazwa kwa ugonjwa wa Ebola kama hakuna kinachofanyika.

« Kuna shirika la madaktari wasio na mipaka ambalo limehamisha wafanyakazi wake, na pia shirika la ALIMA pia limehamisha wafanyakazi wake. Ni kusema vituo vya matibabu vya Ebola vya Katwa na Butembo havifanyi kazi tena. Ni jambo ambalo linakwamisha kazi za kuzuia Ebola. Ikiwa  hakuna kinachofanyika, Ebola itasambaa miongoni mwa wakazi. »

Ifahamike kwamba Wizara ya Afya imeripoti visa vipya 6 vya Ebola mjini Katwa.