Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashauriano ya kijamii DRC yaenda sambamba na harakati dhidi ya Ebola

 Kikundi cha UNICEF kinachoelimisha wananchi  kuhusu Ebola kinahutubia watu wa Beni Kivyu Kaskazini  mashariki mwa DRC.
© UNICEF/UN0228985/Naftalin
Kikundi cha UNICEF kinachoelimisha wananchi kuhusu Ebola kinahutubia watu wa Beni Kivyu Kaskazini mashariki mwa DRC.

Mashauriano ya kijamii DRC yaenda sambamba na harakati dhidi ya Ebola

Afya

Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hadi kufikia jana ni 679 ikiwa ni ongezeko la vifo 37 tangu siku 5 zilizopita.

Mkurugenzi Msaidizi wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, anayehusika na hatua za dharura, Dkt. Ibrahima-Soce Fall amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka Butembo jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Amesema idadi hiyo ni kati ya visa 1089 vilivyoripotiwa tangu mlipuko huo uanze mwezi Agosti mwaka jana ambapo 1023 vimethibitishwa.

Dkt. Fall ametaja maeneo ya Butembo na Katwa kuwa ndio yenye visa zaidi vya Ebola akisema suala la ukosefu wa usalama linasababisha mkwamo wa operesheni za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Akifafanua amesema kuwa, “nina hakika kila mtu anafahamu ongezeko tuliloshuhudia wiki iliyopita ambapo tulikuwa na wagonjwa  72 ikilinganishwa na wagonjwa 56 wiki iliyopita.  Kwa bahati mbaya hiki ni kitu ambacho tulitegemea kwa sababu ukitazama katika wiki tatu zilizopita za kipindi cha kusubiria, tulikuwa na mambo  kadhaa yaliyokwamisha operesheni zetu yakihusiana na usalama, ghasia na mengineyo.”

Amesema ni kutokana na mazingira hayo, watu ambao walikuwa hatarini kupata Ebola, hawakuweza kufikiwa kwa kupatiwa chanjo, hawakuweza pia kuepushwa na maiti za watu waliokufa kutokana na Ebola.

Hata hivyo amesema kuna hatua muhimu wamechukua katika mazungumzo na jamii ili kuhakikisha wanaelewa juu ya athari ya Ebola wakati huu ambapo jamii hizo zimezingirwa na matatizo lukuki ikiwemo ukosefu wa usalama, maji, elimu.

Amesema “ndio maana tumeanzisha mazungumzo ya kijamii kuwasikiliza, kuelewa matatizo yao na kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia na UNICEF ili kushughulikia matatizo ambayo wamekuwa nayo miaka kadhaa.”