Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen inakabiliwa tena na ugonjwa wa kuhara na kipindupindu-WHO na UNICEF.

Mgonjwa wa kipindupindu akipata matibabu katika hospitali ya Al-Sadaqah, Aden, Yemen (Agosti 2018)
OCHA/Matteo Minasi
Mgonjwa wa kipindupindu akipata matibabu katika hospitali ya Al-Sadaqah, Aden, Yemen (Agosti 2018)

Yemen inakabiliwa tena na ugonjwa wa kuhara na kipindupindu-WHO na UNICEF.

Afya

Taarifa kutoka kwa Geert Cappelaere mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika pamoja na Dkt Ahmed Al Mandhari Mkurugenzi wa Shirika la afya duniani kanda ya Medterania Mashariki iliyotolewa mjini Muscat Oman, Amman Jordan na Cairo Misri inasema nchini Yemen, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi tarehe 17 mwezi huu wa Machi, takribani watu 109,000 wamekumbwa na ugonjwa wa kuhara na pia vifo 190 vilihisiwa kusababishwa na kipindupindu tangu mwezi Januari.

Takribani theluthi moja ya wagonjwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano. Hali hii inakuja miaka miwili tangu Yemen iliposhuhudia mlipuko  mkubwa kabisa duniani wa ugonjwa wa kuhara na kipindupindu ambapo zaidi ya watu milioni moja waliporitiwa kupatwa na ugonjwa huo.

Taarifa imewanukuu wawili hao wakisema, “tunahofia kuwa idadi ya maambukizi ya ugonjwa unaosadikika kuwa kipindupindu itaendelea kuongezeka kutokana na msimu wa mvua kuanza mapema na pia huduma za msingi zikiwemo mifumo ya utunzaji maji na miundombinu kuwa imeharibika. Hali inafanywa kuwa mbaya zaidi na mfumo duni wa udhibiti maji taka, matumizi ya maji machafu katika shughuli za kilimo, umeme usioaminika kwa ajili ya kutunza chakula na pia familia kukosa makazi kutokana na kuyakimbia machafuko hususani katika mji wa Hodeida na Tai’z.”

Aidha wamesema timu zao nchini Yemen zinafanya kazi usiku na mchana zikiwa na mtandao mpana wa wadau wa Yemen ili kupambana na kudhibiti kuenea na kuambukiza kwa magonjwa hayo. Wakilenga wilaya 147, vifaa tiba, maji na vifaa vya kujisafi vinakusanywa.

Vikosi vya kudhibiti magonjwa tayari vimetumwa kati maeneo hayo. Jumla ya vituo 413 vya kudhibiti ugonjwa wa kuhara na pia vituo vya kuwapatia maji maalumu walioathirika vinafanya kazi katika wilaya 147 za kipaumbele. Taarifa inasema mzunguko wa kampeni ya chanjo inayotolewa kwa njia ya mdomo ili kuidhibiti kipindupindu  imewafikia watu 400,000 katika wilaya kadhaa. Hadi kufikia sasa ukuzaji uelewa katika jamii umewafikia watu 600,000 katika kampeni ya nyumba kwa nyumba tangu mwaka 2019 ili kuzielimisha familia suala la usafi na kuboresha mfumo wa kuripoti dalili na kutafuta tiba. 

“UNICEF na WHO wamejizatiti kuendelea kuongeza ushiriki katika kusaidia mara moja watu ambao wameathirika na pia kuzuia ugonjwa kusambaa zaidi. Tunafanya kila liwezekanalo kuepuka hali kama yam waka 2017 ikiwemo kwa kuchukua hatua za haraka na pia chanjo ya kipindupindu. Hata hivyo tunakumbana na changamoto kadhaa zikiwemo mapigano yanayoendelea, kutoweza kufikia katika baadhi ya maeneo na urasimu wa kuweza kuingiza misaada ya kuokoa maisha na pia wafanyakazi wetu nchini Yemen.” Wamesema.

Na ICRC waguswa

Wakati hayo yakijiri, kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC imesema mapigano mapya yanayoibuka nchini Yemen yanahatarisha maisha ya watu ambao tayari wamechoka, wana njaa na wamechoshwa na vita.

Taarifa ya ICRC iliyotolewa hii leo nchini Yemen na pia Geneva Uswisi inasema miaka minne baa ya kuanza kwa mgogoro nchini Yemen na miezi michache baada ya makubaliano yaliyoleta matumaini katika nchi iliyosambaratishwa na vita, kuanza tena kwa mapigano vinawalazimisha watu kuhama na kuifanya nchi kutoka katika hali mbaya kwenda katika hali mbaya zaidi.

Mkuu wa wajumbe wa ICRC nchini Yemen Franz Rauchenstein, anasema,” pamoja na matumaini wiki chache zilizopita, maisha ya mamilioni yay a wayemen yamekuwa magumu. Mapigano mapya yanaiharibu zaidi hali ambayo tayari imeshakuwa mbaya.”

Wiki hii ICRC kwa haraka wametuma tani 7 za vifaa tiba pamoja na timu ya wataalamu ili kudhibiti hali katika hospitali ya Al Mudhaffar mjini Taiz. Katika eneo la Hajja, ICRC inasambaza chakula na vifaa vya nyumbani kwa zaidi ya watu 1,640 ambao wamepoteza makazi kutokana na mapigano ya hivi karibuni.

Aidha ICRC inawasiliana na pande zote zinazohusika katika mgogoro iliu kuwakumbusha wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa.