Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo Yemen kumalizika kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhan

Mtoto muathirika wa kipindupindu anapatiwa matibabu katika kituo cha afya nchini Yemen. Picha: UNICEF

Chanjo Yemen kumalizika kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhan

Afya

Umoja wa Mataifa unasema harakati za kutokomeza Kipindupindu nchini Yemen zinatia moyo.

Kampeni ya kwanza ya chanjo dhidi ya kipindupindu inaendelea huko Yemen na inatarajiwa kumalizika kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Shirika la afya ulimwenguni WHO linasema kampeni hiyo iliyoanza tarehe 6 mwezi huu inalenga kuzuia kuibuka tena kwa mlipuko wa gonjwa hilo ambalo tangu mlipuko wake mwaka mmoja uliopita visa zaidi ya milioni moja vimeripotiwa.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen Dkt. Nevio Zagaria amesema gonjwa hilo linashamiri kutokana na ukosefu wa huduma za kujisafi, maji safi pamoja na mifumo ya majitaka.

Mamlaka za afya Yemen pamoja na WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF ndio wanatekeleza kampeni hiyo itakayofunga pazia tarehe 15 mwezi huu.

Tarehe 24 mwezi uliopita, UNIEF iliwasilisha awamu ya kwanza ya dozi 455,000 za chanjo ya kipindupindu kutoka ubia wa chanjo duniani, GAVI.

Walengwa kwenye kampeni hiyo inayohusisha wilaya tano ni watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja bila kusahau wajawazito.

Kampeni inafanyika nyumba kwa nyumba.

TAGS: WHO. Kipindupindu, Yemen