Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila yanayowakabili raia Hodeidah Yemen hayaelezeki:Grande

Mtoto anayeugua unyafuzi katika hospitali ya  Al-Thawra, Hodeidah, Yemen
UNICEF/Abdoo Al-Karim
Mtoto anayeugua unyafuzi katika hospitali ya Al-Thawra, Hodeidah, Yemen

Madhila yanayowakabili raia Hodeidah Yemen hayaelezeki:Grande

Amani na Usalama

Wiki moja baada ya mapigano kuanza kwenye uwanja wa ndege katika mji wa bandari wa Hodeidah, maelfu ya raia wamesalia katika hatari kubwa hali ambayo inalitia hofu kubwa shirikala Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA.

Kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu na mkuu wa OCHA nchini Yemen Lise Grande, hata kabla ya kuzuka upya machafuko hayo hali mjini Hodeidah ilikuwa mbaya sasa imekuwa ni kama kuweka msumari wa moto juu ya kidonda na hasa kwa watoto. Jens Learke ni msemaji wa OCHA Geneva

(SAUTI YA JENS LEARKE)

“Asilimia 25 ya watoto Hodeida wanaumwa unyafuzi, endapo msaada wa lishe kutoka kwa wadau wa masuala ya kibinadamu itaingiliwa itahatarisha maisha ya watoto takriban 100,000. Hodeida ilikuwa moja ya vitovu vya mlipuko wa kipindupindu mwaka jana ambao ulikuwa mbaya kaabisa katika historia sasa”

Bi Grande amesema kiwangio na kiasi cha madhila kwa binadamu Hodeida kinatia uchungu mkubwa na hakisemeki. Hata hivyo ameongeza kuwa wahudumu wa kibinadamu wamekuwepo eneo hilo wakigawa misaada na wataendelea kuwepo endapo mazingira yataruhusu.

Baadhi ya misaada wanayotoa ni pamoja na maboksi ya chakul na vifaa vya dharura kwa familia zilizotawanywa, pia wameweka mafuta ya kutosha kusaidia kusukuma mtambo wa maji kwa ajili ya hospitali, mimea na kila siku wanasaidia kutoa lita zaidi ya milioni 46 za maji.

Umoja wa Mataifa unauchukulia mgogoro wa Yemen kama ndio mbaya zaidi wa kibinadamu duniania na kutoa wito kwa pande zote katika mzozo kufanya kila liwezekanalo kuwalinda raia na miundombinu yao mjini Hodeida ambako ndio lango la kuingilia misaada ya kibindamu nchini Yemen.