Hali ya afya kwa maelfu Hodeidah, Yemen ni mtihani mkubwa

Hali ya afya Hodeidah, ambayo hata kabla ya machafuko ilikuwa tete sasa iko njia panda limeonya leo shirika la afya duniani WHO.
Kwa mujibu wa WHO visa vya maradhi ya kuambukiza ya kipindupindu, donda koo na surua vimeongezeka na vinaendelea kuzuka kila uchao japo kwa kasi ndogo , na kufuatia mapigano yanayoendelea katika mji huo wa bandari, huduma ziko njiapanda na kuwafanya maelfu ya waathirika kuwa hatarini.
Visa vya kipindupindu sasa ni zaidi ya 163,000, donda koo zaidi ya 200 na visa vinavyoshukiwa kuwa surua ni zaidi ya 250. Asilimia 70 ya watu ambao wanategemea huduma za afya Hodeidah na msaada mwingine unaoingia Yemen kupitia bandari ya mji huo, hatma yao iko mashakani ikiwa ni pamoja na watu wa majimbo mengine ya Kaskazini mwa nchi hiyo, limesema shirika la WHO.
Ingawa mapigano yamepungua kasi mjini humo na bandari inaendelea kufanya kazi , lakini bado ukosefu wa usalama unaleta changamoto. Kati ya Juni 13 na Julai 7 mwaka huu watu 328 wamejeruhiwa na wengine 46 kupoteza maisha .
Pia kiwango cha utapia mlo Hodeidah kimeelezwa kuwa cha juu kabisa nchini humo na kufikia asilimia 25.5 , kwa sasa kuna vituo 7 vinavyofanya kazi ya kutoa lishe mjini humo na vingine 7 katika majimbo mengine.
Tangu mwanzo wa wiki hii WHO imepeleka tani 100 za vifaa zikiwemo dawa ambazo zitawasili hivi karibuni kwa njia ya meli kutoka Djibouti hadi Al Hudaydah.
Msaada mwingine unaotolewa na WHO ni pamoja na mafuta ya magari, vitanda vya wagonjwa na magodoro, pia WHO inaendesha huduma ya magari 7 ya kubeba wagonjwa katika hospitali sita, inatoa lita 450,000 za maji katika hospital tatu na kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wahudumu wa afya 100 kwenye maeneo yaliyoathirika na vita.