Chanjo dhidi ya Kipindupindu yaendelea Yemen

2 Oktoba 2018

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanashirikiana na serikali ya Yemen katika kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu, OCV, ili kuepusha mlipuko wa tatu wa ugonjwa huo nchini humo.

Chanjo hiyo iliyoanza kutolewa tarehe 30 mwezi uliopita itaendelea  hadi tarehe 3 mwezi huu wa Oktoba ambapo mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa usaidizi ni pamoja na lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO.

Maeneo lengwa ni wilaya za Al-Hali na Al Marawiah jimboni Hudaydah na wilaya ya Hazm Al Udayn jimboni Ibb, maeneo ambayo awamu kwanza ya chanjo dhidi ya kipindupindu ilifanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi Tarik Jasarevic amesema katika kampeni ya awali walifanikiwa kuwapatia chanjo asilimia 72 ya walengwa ambao in kuanzia watoto wenye umri wa mwaka mmoja.

“Yemen inakabiliwa na milipuko hatari zaidi ya Kipindupindu katika zama za sasa. Tangu Aprili mwaka 2017 zaidi ya watu milioni 1.2 wameshukiwa kuwa na ugonjwa huo ambapo kati yao zaid ya 2,500 wamefariki dunia. Asilimia 96 ya majimbo ya Yemen yameathiriwa na Kipindupindu ikimaanisha ni majimbo 22 kati ya 23. Na asilimia 92 ya wilaya zote zina ugonjwa huo,” amesema Bwana Jasarevic.

Kwa mujibu wa WHO kuna ongezeko la visa vinavyoripotiwa vya Kipindupindu tangu mwezi Juni mwaka huu hususan wiki iliyopita, ikimaanisha kuwa kuna ongezeko la ugonjwa huo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud