Wahisani fungueni zaidi mikoba yenu mnusuru Ebola DRC - Dkt. Tedros

26 Februari 2019

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametaka ufadhili zaidi wa harakati za kutokomeza mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Dkt. Tedros amesema kuna mahitaji ya dharura ya dola milioni 148 kusaidia wadau wote kufanikisha operesheni zao dhidi ya Ebola huko Mashariki mwa DRC lakini hadi sasa kilichopatikana ni dola milioni 10 pekee.

Taarifa ya WHO imesema Dkt. Tedros ametoa wito huo wakati huu akijiandaa kufanya ziara nchini DRC wiki ijayo ambako atakutana na Rais Felix Tshisekedi mjini Kinshasa kabla ya kusafiri kuelekea maeneo yaliyokumbwa na Ebola huko Butembo na Katwa.

“Hali ni ya aina yake, katu hakujakuwepo na  mlipuko wa Ebola kwenye mazingira kama haya ambapo kuna misafara mingi ya watu sambamba na mapengo ya utoaji wa huduma za afya,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema hofu nyingine ni hali ya usalama ambapo amesema anatiwa hofu kubwa na taarifa ya kwamba kituo cha afya kinachoendeshwa na madaktari wasio na mipaka, MSF huko Katwa kimeshambuliwa jumapili usiku.

Hata hivyo amesema licha ya changamoto hizo, kutokana na ushirikiano na serikali na wadau, mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuwa mamia ya vifo vimeepukwa.

Amerejelea kuwa mlipuko bado haujaisha na hivyo fedha zahitajika kusaidia kampeni za kutokomeza ugonjwa huo ulioripotiwa mwezi Agosti mwaka jana.

Zaidi ya watu 80,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola kupitia vituo zaidi ya 400 huku maelfu ya visa vipya vinavyoshukiwa vinafuatiliwa.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter