Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola bado ni changamoto tunayokabiliana nayo DRC-WHO

UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.

Ebola bado ni changamoto tunayokabiliana nayo DRC-WHO

Afya

Mlipuko wa 10 wa Ebola ulioikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, umeendelea kuwa changamoto kwa serikali ya nchi hiyo, Umoja wa Mataifa na wadau wengine wanaosaidia kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo hatari.

Katika tathimini iliyotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni WHO kuhusu hali ya Ebola DRC, shirika lolo limesema kwa kushirikiana na serikali ya DRC na wadau wengine wanaendelea kukabiliana na mlipuko huo licha ya changamoto za kiusalama na jamii kutokuwa na Imani.

Wagonjwa wapya

Thomas Kakule Manole alinusurika kuambukizwa ebola na hapo anaangalia mwanae wa wiki moja, Benedicte, katika chumba cha kutengwa cha matibabu ya ebola Mashariki mwa Kongo, mkewe Thomas alifariki kurokana na ebola na sasa mwanae anaumwa ebola.
© UNICEF/UN0264163/Hubbard
Thomas Kakule Manole alinusurika kuambukizwa ebola na hapo anaangalia mwanae wa wiki moja, Benedicte, katika chumba cha kutengwa cha matibabu ya ebola Mashariki mwa Kongo, mkewe Thomas alifariki kurokana na ebola na sasa mwanae anaumwa ebola.

WHO inasema katika wiki za karibuni kumeripotiwa idadi kubwa ya visa vipya vya Ebola viliochangiwa na mlipuko katika eneo la Katwa ambako Umoja wa Mataifa na wadau sasa wameelekeza nguvu zao kuudhibiti ikijumuisha Benin a Oicha ili kuhakikisha mlipuko huo hausambai Zaidi.

Akizungumza mjini Geneva katika tathimini hiyo mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Motshidisho Moeti amesema licha ya kudhibiti kusambaa kwa mlipuko huo timu za wauguzi na wataalamu wa afya zitafanya juhudi kubwa kujenga Imani ya jamii na ushiriki wao katika vita dhidi ya ugonjwa huu kwenye maeneo yaliyoathirika.

Idadi ya visa vya Ebola

Kwa mujibu wa WHO ikikaribia miezi sita tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola DRC, kumekuwa na jumla ya visa 752, kati ya hivyo 698 vimethibitishwa na 54 vikidhaniwa. Kwa upande wa vifo kufikia 29 Januari mwaka huu ni asilimia 62 ya wagonjwa wote sawa na watu 465. Hata hivyo watu wengine 259 wametibiwa kwenye vituo maalumu vya Ebola na kuruhusiwa kurejea nyumbani na visa hivyo Zaidi vilikuwa miongoni mwa wanawake chini ya umri wa miaka 18 na watoto 115 waliokuwa na umri wa chini ya miaka mitano. Na katika siku 21 zilizopita WHO inasema kumeripotiwa visa vipya 118 kwenye vituo 11 vya afya maeneo ya Katwa, Beni, Butembo, Kayina, Oicha, Manguredjipa, Biena, Kyondo, Musienene, Komanda na Vuhovi.
 

Tathmini ya WHO kuhusu hatari ya Ebola 

WHO imefanya tathimini kuhusu hatari ya mlipuko wa Ebola na kusema bado iko juu sana katika ngazi ya taifa na kikanda, lakini katika ngazi ya kimataifa hatari bado ni ndogo. Na shirika hilo limesema maeneo yaliyoathirika Zaidi ni majimbo ya Kaskazini Mashariki mwa DRC yanayopakana na Uganda, Rwanda na Sudan Kusini. Na hari ya kusambaa ni kubwa kutokana na watu kusafiri kati ya  maeneo yaliyoathirika kwenda sehemu zingine za nchi nan chi jirani. Lakini hatari pia inachochewa na kwamba nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya usalama. Pia DRC hivi sasa kuna mlipuko wa kipindupindu na tatizo la malaria.

Ushauri wa WHO kuhusu Ebola

Kimataifa WHO inashauri kusiwe na vikwazo vyovyote vya usafiri kwenda DRC n ahata biashara na taifa hilo kutokana na taarifa zilizopo. Pia shirika hilo limesema hadi sasa hakuna chanjo iliyohalalishwa na kupewa leseni ya kuwalinda watu dhidi ya virusi vya Ebola hivyo mahitaji yoyote ya vyeti vya chanjo ya Ebola sio ya msingi kwa kuzuia watu kusafiri mipakani au kutoa pasi za kusafiria kwa wasafiri wanaoondoka DRC. Hivyo WHO inaendelea kufuatilia kwa karibu na endapo itahitajika kuthibitisha safari na hatua za biashara zinazohusiana na mlipuko huo.

Vikwazo vya usafiri

WHO inasema hadi sasa hakuna nchi yoyote ambayo imetekeleza hatua za vikwazo vya usafiri inayoingilia safari za kimataifa za kwenda na kutoka DRC. Hata hivyo shirika hilo limewashauri wasafiri kupata ushauri wa kitabibu kabla ya kusafiri na kutekeleza masharti ya usafi.