Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku chache kabla ya DRC kutangaza mwisho wa Ebola, mgonjwa mpya agundulika

Mkurugenzi mkuu wa WHO Adhanom Ghebreyesus alipozuru Butembo nchini DRC Aprili mwaka 2019 baada ya watu wenye silaha kushambulia kituo cha Ebola
WHO/Junior Kannah
Mkurugenzi mkuu wa WHO Adhanom Ghebreyesus alipozuru Butembo nchini DRC Aprili mwaka 2019 baada ya watu wenye silaha kushambulia kituo cha Ebola

Siku chache kabla ya DRC kutangaza mwisho wa Ebola, mgonjwa mpya agundulika

Afya

Siku chache kabla ya ulimwengu kutangaza kuutokomeza ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,  Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa twitter Ijumaa ya leo, kwa masikitiko ametangaza kubainika kwa mgonjwa mpya wa Ebola nchini humo.

Kwa mujibu wa utaratibu wa milipuko ya magonjwa duniani, ambapo baada ya siku 42 kupita bila mgonjwa yeyote kubainika, Jumatatu ya wiki ijayo DRC ilikuwa itangaze kuutokomeza ugonjwa wa Ebola lakini kutokana na kisa hiki kipya haitaweza kufanya hivyo.

Dkt Ghebreyesus amesema, “leo nimefanya mkutano wa kamati ya dharura kuhusu Ebola nchini DRC. Baada ya siku 52 bila mgonjwa yeyote, timu ya uchunguzi huko DRC imethibitisha mgonjwa mpya. Tumekuwa tukijiandaa na tunategemea wagonjwa zaidi.”

Tweet URL

 

Aidha Dkt Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa Twitter ameeleza kwa masikitiko kuwa ni bahati mbaya kuwa hali hii inamaanisha serikali ya DRC haitaweza kutangaza kufikia kwa ukomo wa mlipuko wa Ebola Jumatatu kama ilivyotumai na akaongeza, WHO inabaki DRC na imejizatiti kama kawaida kushirikiana na serikali, jamii zilizoathirika na wadau ili kutokomeza Ebola.”

Mlipuko wa hivi sasa ambao ulitangazwa mnamo tarehe mosi ya mwezi Agosti 2018, ni wa kumi katika nchi ya DRC na wa pili kwa ukubwa kidunia baada ya ule wa mwaka 2014 hadi 2016 huko Afrika Magharibi.

Hadi kufikia tarehe mosi ya mwezi Machi,2020 kulikuwa na vifo 2264 vilivyosababishwa na Ebola nchini DRC.

Mnamo tarehe 4 ya mwezi Machi mwaka huu wa 2020, WHO ilikuwa imetoa iliyooiita habari njema kuwa mgonjwa wa mwisho wa Ebola nchini DRC ameruhiswa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu katika kituo cha matibabu huko kaskazini mashariki mwa mji wa Beni. Kisa hiki kipya cha sasa kinairudisha timu nzima ya WHO na wadau wake katika mapambano makali dhidi ya Ebola.