Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasema itasalia Butembo, DRC mpaka itakapotokomeza ebola

Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.

WHO yasema itasalia Butembo, DRC mpaka itakapotokomeza ebola

Afya

Viongozi wakuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO wamekamilisha ziara yao ya siku mbili kwenye mji wa Butembo, mji ulioathirika zaidi na ugonjwa wa Ebola kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. 

(Nats)

Ndege iliyobeba viongozi wa WHO akiwemo mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Dkt. Tedros Ghebreyesus na mkurugenzi WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti ambao wametembelea mji wa Butembo, huku wakikaribishwa kwa salamu za aina  yake kwenye eneo hili lililobeba mzigo mkubwa wa ebola.

Walitembelea na kuona mshikamano na kushukuru wafanyakazi wa WHO na wadau huku wakitathmini hatua zinazohitajika kuimarisha usalama na juhudi za kukabilia na ebola.

Aidha wamekutana na viongozi wa kisiasa, biashara na kidini wa eneo hilo na kutoa wito wa kufanya hima kuimarisha juhudi za kuboresha mazingira ambapo Bwana Tedros amesema,

(Sauti ya Tedros)

“Kama mjuavyo idadi ya wagonjwa hususan Butembo na Katwa inaongezeka kwa asilimia 20 kila siku, hii ni hatari sana, na tuna wasiwasi sana na najua mna wasiwasi pia.”

Kwa mujibu wa WHO, juhudi za kukabiliana na ebola ikiwemo kushirikisha jamii, utoaji chanjo na uchunugzi wa wagonjwa  umezinduliwa upya baada ya kusimamishwa kwa muda baada ya mauaji ya daktari wa WHO na kujeruhiwa kwa watu wawili.

Hata hivyo WHO imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa visa vipya katika wiki za hivi karibuni ambapo Dkt. Moeti amesema

“Tunajizatiti kusalia hapa, na nimetiwa moyo sana na dhamira ya wafanyakazi wenzangu ambao wako hapa kuendelea na vita hivi na ilinigusa kwamba licha ya machungu walio nayo walifurahi na walitiwa moyo na uwepo wetu hapa na wamedhamiria kusonga mbele. Kwa hiyo tuko hapa mpaka pale tutaweka kikomo kwa janga hili.”

WHO imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuimarisha misaada wakati huu ambapo ni nusu tu ya ombi lililotolewa limefadhiliwa hali ambayo huenda ikapelekea WHO na wadau kusitisha baadhi ya shughuli zake.