Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa ebola DRC mashariki ni wa pili kwa ukubwa katika historia

Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018
UNICEF/Guy Hubbard
Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018

Mlipuko wa ebola DRC mashariki ni wa pili kwa ukubwa katika historia

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema mlipuko wa ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni wa pili kwa ukubwa duniani na umeathiri zaidi watoto. 

Mlipuko wa hivi karibuni zaidi huko mashariki mwa DR Congo ulitangazwa tarehe Mosi mwezi Agosti mwaka jana ambapo UNICEF inasema kati ya watu 740 waliothibitishwa kuugua  ugonjwa huo, asilimia 30 ni watoto.

Zaidi ya hao watu 460 kati yao walifariki dunia huku 258 walinusurika ugonjwa huo. 

UNICEF inasema mlipuko huu ni wa 10 kutokea nchini DRC na ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo na ni wa pili kwa ukubwa kuwahi kushuhudiwa kwenye historia ukiongozwa na mlipuko wa ebola huko Afrka Magharibi kati ya mwaka 2014-2016.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, dokta Gianfranco Rotigliano, amesema wameimarisha juhudi ili kudhibiti kuenea kwa Ebola huo, kusaidia wathirika an hatimaye kutokomeza kabisa mlipuko huo.

Amesema licha ya kuwepo mafanikio makubwa ya kudhibiti Ebola katika maeneo ya Mangina, Beni na Komanda, bado unaenea katika maeneo yasiyo na usalama ya Butembo kutokana na mzozo na usafiri wa watu usiodhibitiwa.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imetuma wafanyakazi zaidi kwenye vituo vya afya kule Butembo na Kutwa ambako 65% ya visa vipya vya Ebola vimeripotiwa katika majuma matatu yaliopita.

UNICEF inajikita katika ushirikishwaji wa jamii, kutoa huduma za maji na usafi, kuhakikisha kuna mazingira salama ya watoto shuleni na kusaidia watoto na familia zilizoambukizwa ama kuathirika.

Watoto wakijifunza jinsi ya kujilinda na Ebola huko nchini DR Congo katika eneo la Beni
UNICEF/UN0235949/Nybo
Watoto wakijifunza jinsi ya kujilinda na Ebola huko nchini DR Congo katika eneo la Beni

UNICEF ikitoa ripoti hiyo, naye Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani amenukuu shirika la afya ulimwenguni, WHO akisema kuwa bado kuna ongezeko la visa vya ebola

(sauti ya Dujarric)

“Kumekuwa na ongezeko la visa vya ebola katika jimbo la kivu kaskazini nchini DRC, hususan kwenye eneo la Katwa ambapo timu za kukabiliana na mlipuko zimekumbwa na ukosefu wa imani kutoka kwa wanajamii, mlipuko umekwenda hadi maneoe ya Kayina ambako hali ya usalama ni hatarishi.”

Bwana Dujarric ameongeza kuwa WHO inajizatiti kujenga upya imani ya jamii na kuimarisha juhudi za kukabiliana na mlipuko huo katika maeneo hayo.