Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamlaka sahihi ya ulinzi wa amani DRC ni muhimu ili kuimarisha usalama-Tanzania

Wanajeshi wa Tanzania wakiwa wamebeba miili ya wenzao waliouawa wakati wakiwa kwenye  operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa  huko DRC na CAR
UNIC Dar es salaam

Amani na Usalama

Nchini Tanzania hii leo walinda amani watatu wa taifa hilo waliouawa katika matukio tofauti ya mapigano huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wameagwa rasmi katika tukio lililoongozwa na Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi.

Walinda amani hao wanahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO na huko CAR, MINUSCA.

Katika tukio la huko Beni, jimbo la Kivu Kaskazini, nchini DRC, Private Mussa Shija Machibya ambaye ni komando, aliuawa wakati wa mapigano na waasi wa ADF ilhali mwenzake Koplo Mohammed Mussa alifariki kwenye ndege wakati akipelekwa huko Entebbe nchini Uganda kwa matibabu zaidi baada ya kujeruhiwa kwenye mapigano hayo. Wawili  hao walikuwa wanahudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB ambacho  kina askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

Jijini Dar es salaam nchini Tanzania, askari wa Tanzania wakifanya gwaride kuzunguka majeneza ya wenzao watatu waliouawa wakati wakilinda amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Mlinda amani mwingine, Koplo Erick Masauri John aliuawa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati wa makabiliano na vikundi vilivyojihami.

Akizungumza katika tukio la kuaga miili ya walinda amani hao Waziri wa Ulinzi Dkt Mwinyi amesema, "wakati umefika kwa operesheni zote za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zifanye kazi kwa mujibu wa ibara ya 7 ya katiba  ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa huko DRC, Tanzania, Malawi na Afrika Kusini zinatekeleza operesheni za ulinzi wa amani kwa mujibu wa ibara ya 6. Wakati umefika operesheni zote zifanye kazi chini ya ibara moja."

Naye mnadhimu mkuu wa jeshi la ulinzi wa wananchi la Tanzania,  TPDF Luteni Jenerali Yakubu Hassan Mohamed amesema licha ya matukio hayo Tanzania itaendelea na ulinzi wa amani.

Tanzania ni ya tisa duniani kwa kuchangia idadi kubwa ya askari na wanajeshi kwenye operesheni za ulinzi  wa amani za Umoja wa Mataifa.