Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa utaendelea kushikama na CAR licha ya mashambulizi:Guterres

Doria zikiendelea kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui na viunga vyake huku wananchi wakiendelea na shughuli zao. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Umoja wa Mataifa utaendelea kushikama na CAR licha ya mashambulizi:Guterres

Amani na Usalama

Licha ya mashambulizi ya wiki hii nchini Jamhurui ya Afrika ya Kati , CAR  Katibu Mkuu wa Umoja wa Msataifa Antonio Guterres amesema hii leo anashikamana na taifa hilo na kuonya kwamba mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia wasioweza kujitetea na walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wake  Stephane Dujarric inasema “Katibu Mkuu anahofu kubwa kufuatia kuongezeka kwa machafuko katika siku za karibuni  nchini CAR”

Bwana. Guterres ameyasema hayo baada ya shambulio la Alhamisi Novemba 15 kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Alindao, kilometa 300 Mashariki mwa mji mkuu Bangui. Takriban watu 37 waliuawa kwenye shambulio hilo lililotekelezwa na kundi lenye silaha la Muungano kwa ajili ya amani Jamhuri ya Afrika ya Kati , UPC.

Katika shambulio lingine tofauti jana Ijumaa kwenye kituo cha mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo , MINUSCA katika eneo la Kusini Magharibi mwa mji wa Gbambia , mlinda amani kutoka Tanzania aliuawa. Kwa mujibu wa taarifa ya Guterres shambulio hilo linakisiwa kufanywa na kundi lenye silaha la Siriri.

Walinda amani wa Umoja wa Mastaifa walikuwa wakiwalinda raia waliokuwa wanapata hifadhi kwenye Kijiji cha Gbambia waliposhambuliwa. Mlinda amani wa Tanzania alijeruhiwa na kufariki dunia baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na serikali ya Tanzania. Pia amesema anaendelea kushikamana na watu na serikali ya CAR.

Katibu Mkuu amekumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na raia wasioweza kujitetea yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Ametoa wito kwa mamlaka ya CAR kuchunguza mashambulizi hayo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mbele ya sharia.

Katibu Mkuu amerejelea kusema MINUSCA imejizatiti kulinda raia na kuchangia katika utulivu wa taifa hilo .

CAR imeghubikwa na machafuko tangu kuzuka kwa mapigano baina ya wanamgambo wa Kikristo wanaojiita anti-Balaka na muungano wa wapigakaji wa Kiislamu wa Seleka mwaka 2012.

Wakati mkataba wa amani ulifikiwa Januari 2013, waasi walidhibiti mji mkuu Bangui mwezi Machin na kulazimisha Rais Francoise Bozize kukimbia.

Kufuatia hofu ya usalama, masuala ya kibinadamu, haki za binadamu, mgogoro wa kisiasa na athari zake kwenye ukanda mzima, MINUSCA ilianza operesheni zake mwaka 2014 chini ya kifungu cha VII cha katika ya Umoja wa Mataifa.

Wakati ulinzi wa raia ukiwa ndio jukumu lake kuu , kifungu namba VII kinatoa fursa ya kutumia nguvu, ikimaanisha kwa ruksa ya Baraza la Usalama, walinda amani wanaweza kujibu mashambulizi ya vitendo vya kikatili.