Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani saba wa UN wauawa DRC: Wanatoka Malawi na Tanzania

FIB vikosi maalum vya Tanzania ambao wanahudumu katika sehemu ya MONUSCO, huko Sake, North Kivu (Maktaba). Picha: © MONUSCO / Sylvain

Walinda amani saba wa UN wauawa DRC: Wanatoka Malawi na Tanzania

Amani na Usalama

Walinda amani 7 wa Umoja wa Mataifa wameuawa huko Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Taarifa za awali zinasema kuwa walinda amani hao, 6 kutoka Malawi na mmoja kutoka Tanzania, waliuawa wakati wa operesheni ya pamoja kati ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko DRC, MONUSCO na jeshi la serikali, FARDC dhidi ya waasi wa kikundi cha ADF.

Kufuatia ripoti hizo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali kitendo hicho ambacho pia kimeacha walinda amani 10 wakiwa wamejeruhiwa na mmoja hadi sasa hajulikani aliko.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo jijini New  York, Marekani ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Malawi na Tanzania huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Askari wa kikosi cha FIB akishika doaria  Beni Mashariki mwa DRC ambapo UN ilikuwa inasaidia jeshi la serikali katika operesheni zake.
Photo: MONUSCO/Sylvain Liechti
Askari wa kikosi cha FIB akishika doaria Beni Mashariki mwa DRC ambapo UN ilikuwa inasaidia jeshi la serikali katika operesheni zake.

Halikadhalika amesisitiza mshikamano wake na vikosi vya Tanzania na Malawi ambavyo amesema vinafanya kazi katika mazingira magumu ili kulinda raia dhidi ya waasi hao wa ADF na vikundi vingine vilivyojihami.

 
Katibu Mkuu ametoa wito kwa vikundi vilivyojihami kukomesha shughuli zao zinazohatarisha utulivu na usalama ambazo zinazidi kuongeza machungu kwa raia na kukwamisha harakati za kudhibiti mlipuko wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini.

“Natoa wito wasalimishe silaha mara moja na nasihi mamlaka za DRC zichukue hatua za lazima ili kukamata na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa mashambulio dhidi ya raia, jeshi la taifa na walinda amani nchini DRC,” amesema Bwana Guterres.