Skip to main content

SheTrades yaendelea kupanua wigo wake, yabisha hodi Zambia

Mariana Masias katika sekta biashara ya mavazi. Picha: ITC

SheTrades yaendelea kupanua wigo wake, yabisha hodi Zambia

Wanawake

Kituo cha kimataifa cha biashara, ITC leo kimezindua tawi lake nchini Zambia na hivyo kutoa fursa ya kuunganisha wanawake wajasiriamali nchini humo na wenzao duniani kote.

Uzinduzi umefanyika kwenye mji mkuu wa Zambia, Lusaka, siku moja kabla ya kuanza kwa jukwaa la kimataifa la kuendeleza biashara ya nje, WEDF la mwaka huu wa 2018.

Stella Vuzo ambaye ni afisa habari wa Umoja wa Mataifa anayeripoti mkutano huo amemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa ITC Arancha González akisema kuwa “uzinduzi huu utaimarisha uwezo wanawake wajasiriamali nchini Zambia wa kushindana na wajasiriamali wengine kwenye masoko ya kimataifa.”

Zaidi ya hayo, SheTrades Zambia itazindua tathmini ya kusaka kanzi data za kuhusu wajasiriamali wanawake na mahitaji yao mahsusi.

“SheTrades Zambia itafanya kazi kwa ubia na serikali ya Zambia na jumuiya ya wafanyabiashara ili kuweza kufahamu ni jambo gani la kufanya kuongeza ushidani wa bidhaa na hatimaye bidhaa hizo ziweze kupenyeza soko la kimataifa,” amesema Bi. González.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mtendaji huyo wa ITC amesema “mtandao huu unalenga kuchochea ukuaji wa kiuchumi na kupanua fursa za ajira katika biashara zinazoendeshwa na kumilikiwa na wanawake kwa kuongeza dhima yao katika biashara hizo ndani ya Zambia, kwenye kanda ya Afrika na duniani kwa ujumla.”

ITC inasema baada ya kukusanya takwimu na mahitaji mahsusi, wanawake wajasiriamali hao wa Zambia watapatiwa mafunzo kulingana na mahitaji yao sambamba na kufanya kazi na wabobezi ili kujifunza kwa vitendo jinsi ya kuanzisha na kuendesha biashara.

Wanawake wajasiriamali kama huyu wakipatiwa mafunzo ya biashara watakwamua sio tu familia zao bali pia jamii zao
ILO/screen capture
Wanawake wajasiriamali kama huyu wakipatiwa mafunzo ya biashara watakwamua sio tu familia zao bali pia jamii zao

Annette Ssemuwemba, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa EIF, taasisi itakayoshirikiana pia na ITC katika kufanikisha SheTrades Zambia amesema “tuna furaha kubwa ku Kitendo cha wanawake kufikia masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, kinaweza kuwa na athari chanya kubwa za kubadilisha maisha yao na familia zao kuanzia kuondoa umaskini na kukuza kipato. Tunaona SheTrades Zambia itakuwa kichocheo kwa wanawake kuhamasika, kupata taarifa na waleta mabadiliko ya kibiashara.

Ili kufanikisha zaidi mpango huo wa SheTrades, benki ya StanBic Zambia itashirikiana na mpango huo ili kuondokana na changamoto za kijinsia zinazokwamisha ukuaji wa biashara zinazoendeshwa na wanawake.

Mathalani, suala la wanawake kupata mikopo, hivyo benki hiyo itachukua hatua ikiwemo kuelimisha wanawake kuhusu masuala ya fedha na kuwawezesha kushiriki kwenye maonyesho ya kimataifa ya biashara.

SheTrades inayoratibiwa na ITC ambayo ni wakala wa pamoja wa shirika la biashara duniani, WTO na Umoja wa Mataifa, tayari imezinduliwa Nigeria, Kenya na Rwanda na lengo lake ni kuwa imeuganisha wanawake wajasiriamali milioni moja kwenye masoko ulimwenguni ifikapo mwaka 2020.

Wanawake walio chini ya mpango huo hutumia mtandao wa intaneti kuuza au kununua bidhaa kutoka kwa wenzao na hivyo kupata fursa za kutangaza bidhaa zao kutoka popote pale alipo.