Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongeza ushindani wa SMEs ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Ripoti

Wanawake wajasiriamali kama huyu wakipatiwa mafunzo ya biashara watakwamua sio tu familia zao bali pia jamii zao
ILO/screen capture
Wanawake wajasiriamali kama huyu wakipatiwa mafunzo ya biashara watakwamua sio tu familia zao bali pia jamii zao

Kuongeza ushindani wa SMEs ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuelekea siku ya biashara ndogo na za kati, SMEs hapo kesho, Umoja wa Mataifa umetaka uwekezaji zaidi kwenye biashara hizo kwa kuwa ndio msingi wa kufanikisha maleng ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kituo cha biashara cha kimataifa, ITC ambayo ni ofisi tanzu ya kamati  ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, imesema hayo kupitia ripoti yake mpya iliyotolewa wiki hii ikisema kuwa msisitizo ni biashara ndogo na za kati kwa kuzingatia mambo makuu manne.

Mkurugenzi Mtendaji wa ITC Arancha Gonzalez akitaja mambo hayo yaliyomo kwenye ripoti hiyo iliyopatiwa jina Mtazamo wa biashara ndogo na za kati mwaka 2019- fedha nyingi kwa biashara ndogo, kufanikisha SDGs, ametaja mosi ni kwamba kwa kuongeza ushindani wa biashara ndogo na za kati kupitia ongezeko la uwekezaji, wanachochea fursa za ajira na pia ujira na kwamba.

Wachuuzi wa samaki kama hawa huko Mogadishu Somalia wanaweza kunufaika na eneo la biashara huru Afrika iwapo miundombinu sahihi itawekwa.
AU-UN IST/Stuart Price
Wachuuzi wa samaki kama hawa huko Mogadishu Somalia wanaweza kunufaika na eneo la biashara huru Afrika iwapo miundombinu sahihi itawekwa.

 “Namba mbili iwapo tutawekeza kwenye SMEs, itaboresha utendaji wa kibiashara, na uzalishaji endelevu. Tatu, ukiwekeza kwenye SMEs itakuwa na athari chanya kwenye sekta nyingine kama afya, maji chakula na elimu na namba nne itakuwa na matokeo chanye kwenye uchumik wa ndani kwa kuwa na ubunifu zaidi.”

Bi. Gonzales amesema kuwa biashara ndogo na za kati katika nchi zinazoendelea zikipatiwa nyongeza ya dola trilioni 1 zitafanikisha SDGs kwa asilimia 60 wakati huu ambapo pengo la ufadhili ni dola trilioni 5.

Amesema uwekezaji huo wa kuongeza ushindani kwenye biashara ndogo na za kati, utalenga zaidi malengo mawili ambayo ni namba 8 la ajira zenye utu na lengo namba 9 kuhusu ubunifu lakini malengo hayo yana manufaa kwa malengo mengine kama vile kutokomeza njaa, kutokomeza umaskini na usawa wa jinsia.

Takwimu zinaonesha kuwa biashara ndogo na za kati ziwe rasmi au si rasmi zinachangia asilimia 90 ya kampuni zote duniani na kwa wastani huajiri asilimia kati ya 60 na 70 ya nguvu kazi na mchango wake kwenye pato la ndani la nchi ni asilimia 50.