Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamani nataka mananasi na korosho kutoka Tanzania nitazipataje? Ahoji mfanyabiashara kutoka Kenya

Matunda ya mananasi, cha ndani ni tunda na ganda nalo lina faida.
Picha na FAO/Ezequiel Becerra
Matunda ya mananasi, cha ndani ni tunda na ganda nalo lina faida.

Jamani nataka mananasi na korosho kutoka Tanzania nitazipataje? Ahoji mfanyabiashara kutoka Kenya

Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa la kusongesha biashara ya nje, WEDF18 ingawa limefunga pazia huko Lusaka, Zambia, wafanyabiashara wanaendelea kuhaha kusaka taarifa za kupata bidhaa bora ili kuimarisha masoko yao ya nje.

Baada ya kukumbana na shida ya kupata bidhaa za kuuza Ulaya na falme za kiarabu, mfanyabiashara mmoja mwanamke kutoka Kenya amechukua hatua ya kubuni apu ya kumwezesha kuwasiliana na wakulima ili kufanikisha biashara  yake.

Mfanyabiashara huyo Eunice Mbeneka Mutua wa kampuni ya Select Fresh Produce Kenya ltd amemweleza Stela Vuzo wa Kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa wakati wa mahojiano maalum huko Lusaka Zambia kuwa lengo la apu hiyo ni "kuunganisha wakulima na wafanyabiashara ili kuweza kupata taarifa. Bado apu naitengeneza na siwezi kutaja jina lake."

Bi. Mutua ambaye amesoma hadi shahada ya uzamili lakini akaamua kuacha kazi na kujiunga na biashara ya bidhaa za kilimo, anatoa mfano wa jinsi ambavyo alihaha hadi kuchukua uamuzi huo akisema  "nimepata changamoto nyingi sana.  Mfano mimi  nahitaji mananasi na maparachichi kutoka Tanzania na niliwahi kula mananasi yao pale Mwanza yana sukari sana. Kuna watu wanataka hayo mananasi. Pia kuna korosho ambazo zinahitajika huko Marekani. kwa hiyo ni lazima kuona ni jinsi gani tutapata taarifa.  Mkulima akipata taarifa atanufaika na mimi pia nitanufaika."

Jukwaa hilo liliandaliwa na kituo cha kimataifa cha biashara, ITC.