Hatua zachukuliwa ili Ebola isienee nchi jirani na DRC
Shirika la afya duniani WHO, limechukua hatua kuhakikisha ugonjwa wa Ebola uliolipuka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hauingii katika nchi 9 jirani na taifa hilo.
Nchi hizo ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, DRC, Jamhuri ya Congo, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.
Taarifa ya WHO inasema kuwa usaidizi huo unalenga kuimarisha mifumo ya afya ili kuhakikisha iko katika hali ya kuweza kukabiliana na Ebola iwapo utaripotiwa katika nchi hizo.
HATUA PENDEKEZWA
Hatua kama vile kuchunguza, kukinga na kutibu Ebola ndio zinapatiwa msisitizo wakati huu ambapo tayari watu 37 wameripotiwa kufarika kwa Ebola huko DRC kati ya visa 57 vilivyoripotiwa.
Kwa mantiki hiyo WHO inataka mataifa hayo 9 yatathmini uwezo wao wa sasa wa kukabiliana na mlipuko wa Ebola, yabaini upungufu uliopo na hatua zichukuliwe ili kuhakikisha uwezo wa kukabili upo.
Nchi hizo zinaelekezwa mazingira na vifaa vinavyopaswa kuwepo pindi kisa cha kwanza cha Ebola kinaporipotiwa na utayari wa kuendelea kufuatilia.
BAJETI
Kupitia mpango huo WHO itafanya kazi kwa karibu na wizara za afya na wadau wengine ambapo bajeti inayokadiriwa kwa maandilizi hayo kwa miezi tisa ni dola milioni 15.5
Mahitaji ya kila nchi ikiwemo utaalamu wa kiufundi na usaidizi mwingine utatolewa na ofisi za kikanda za WHO pamoja na makao makuu huko Geneva, Uswisi.
TAGS: WHO, Ebola, Tanzania, Uganda, DRC