Ebola imeshabisha hodi Uganda:WHO

11 Juni 2019

Wizara ya afya ya Uganda na shirika la afya ulimwenguni WHO, wamethibitisha kubainika kwa kisa cha virusi vya Ebola nchini Uganda. Ingawa kumekuwa na tahadhari mbalimbali za mlipuko huo nchini humo lakini hiki ni kisa cha kwanza kuthibitishwa Uganda wakati huu ambapo mlipuko wa ugonjwa huo ukiendelea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kisa kilichothibitishwa ni kwa mtoto wa miaka 5 aliyetokea DRC ambaye alisafiri na familia yake na kuingia Uganda Juni 9 mwaka huu kupitia mpaka wa Bwera na kusaka matibabu kwenye kituo cha afya cha hospitali ya Kagambo ambako madaktari walitaja kuwa Ebola ndio ilikuwa chanzo cha kuumwa kwake. Kisha mtoto huyo akahamishiwa kwenye kituo cha matibabu ya Ebola cha Bwera. Uthibitisho wa kuwa ni maradhi ya Ebola umefanyika leo Juni 11 katika taasisi ya virusi ya Uganda (UVRI).

Kwa sasa mtoto huyo anapatiwa huduma na matibabu kwenye kituo cha Ebola cha Bwera na wote aliokutana naye wanaangaliwa na kufuatiliwa kwa ukaribu.

Wizara ya afya ya Uganda na WHO wamepeleka timu maalumu kwenda eneo la Kasese ili kubaini watu ambao watakuwa kwenye hatari na kuhakikisha wanaangaliwa kwa karibu na kupatiwa huduma endapo wataugua.

Uganda ina uzoefu wa kudhibiti milipuko ya Ebola na katika maandalizi ya uwezekano wa kuingia visa vyaugonjwa huo kufuatia mlipuko unaoendelea DRC, Uganda imewapa chanjo karibu wahudumu wa afya 4700 katika vituo 165 ikiwa ni pamoja na katika kituo ambacho hivi sasa mtoto huyo mwenye Ebola anapatiwa matibabu, uchunguzi wa ugonjwa huo umeimarishwa na wahudumu wa afya kupatiwa mafunzo ya kutambua dalili za ugonjwa huo lakini pia vituo vya tiba ya Ebola vimeshaandaliwa.

Katika kukabiliana na kisa hiki kipya wizara ya afya imeongeza elimu kwa umma, msaada wa kisaikolojia na itatoa chanjo kwa wote ambao wamekutana  na mgonjwa huyo na walio katika hatari ikiwemo wahudumu wa afya ambao awali hawakupewa njacho hiyo.

Chanjo ya majaribio iliyotumika DRC na wahudumu wa afya ikiwemo Uganda inaonekana kufanya kazi hadi sasa na kuwalinda watu hao kupata ugonjwa na pia imewasaidia wale waliopata ugonjwa huo kuwa na fursa kubwa ya kuishi, na hivyo serikali imewataka wote waliobainika kukutana na mgonjwa huyo kuchukua hatua za kujilinda.

Uongozi wa wilaya na kata katika eneo lililoathirika umeagizwa kuhakikisha kwamba mtu yeyote mwenye dalili za Ebola katika jamii anaripotiwa kwa wahudumu wa afya haraka iwezekanavyo na kupatiwa ushauri na vipimo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter