Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi ya chanjo dhidi ya Ebola yaanza, licha ya kwamba hakuna Ebola

Uandaaji wa chanjo ya ebola katika maabara hospitali ya Donka, Conakry, Guinea
WHO/S. Hawkey
Uandaaji wa chanjo ya ebola katika maabara hospitali ya Donka, Conakry, Guinea

Maandalizi ya chanjo dhidi ya Ebola yaanza, licha ya kwamba hakuna Ebola

Afya

Nchini Uganda, shirika la afya ulimwenguni, WHO kwa ushirikiana na wizara ya afya wanaendelea na maandalizi ya kuwapatia chanjo wahudmu wa afya na wananchi walio hatarini kukumbwa na ugonjwa wa Ebola iwapo itahitajika kufanya hivyo.

Hatua hiyo imechukuliwa ingawa kwamba  hadi leo nchini Uganda, hakuna uthibitisho wowote wa kuwepo kwa Ebola.

Hata hivyo wahudumu wa afya wameshashughulikia zaidi ya visa 100 shukiwa vya wagonjwa wa Ebola ambapo hakuna hata mmoja amethibitishwa kuwa na Ebola.

Chanjo hiyo itatolewa kwa watu wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo na wale wote ambao walikuwa na makutano au magusano nao, mfumo ambao umekuwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hivi karibuni humo DRC.

Maeneo yenye hatari zaidi ni wilaya 22 za Uganda zilizo mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako hivi karibuni kuliripotiwa tena uwepo wa wagonjwa hususan katika mji wa Butembo, jimboni Kivu Kaskazini.

Mwakilishi wa WHO nchini Uganda, Dkt. Yonas Tegegn Woldermariam amesema tayari miundombinu ya kuhakikisha chanjo 3000 dhidi ya Ebola zinahifadhiwa kwa umakini imekamilika. “Majokofu yenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi chanzo katika kiwango cha nyuzi joto hasi 80 yameingizwa nchini Uganda, bila kusahau jenereta na vyumba vyenye mfumo sahihi wa hewa ambavyo pia vinaweza kutumika pia kwa mafunzo,” amesema DKt. Tegegn.