Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufuatiliaji waimarishwa mpakani kudhibiti mlipuko wa ebola, Uganda na DRC

Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha  muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda
UNHCR/Michele Sibiloni
Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda

Ufuatiliaji waimarishwa mpakani kudhibiti mlipuko wa ebola, Uganda na DRC

Afya

Katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mamlaka wa mpakani nchini humo na wenzao kutoka Uganda wamekubaliana kuimarisha ufuatiliaji wa virusi vya ugonjwa huo kwa kushirikiana zaidi.

Hatua hii imefikiwa katika mkutano uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya na usalama likiwemo shirika la afya ulimwenguni (WHO) na maafisa wa afya wa wilaya za mpakani ambao umefanyika kwenye mpaka wa Kasindi-Luburiha, upande wa DRC.

Kuhusu ukusanyaji wa takwimu, wadau hao wamekubaliana kuoanisha matumizi ya vifaa vya kuchekecha washukiwa wa ebola na kupeana taarifa za ufuatiliaji katika maeneo haya ya mpakani.

Katika mkutano huohuo wa aina yake katika vita dhidi ya ebola mpakani, wamehaha kubaini mipaka yote inayotumiwa na wasafiri ili kutiiwe vituo vya kuwachekecha.

Kwa kutambua umuhimu wa uhamasishaji wa umaa, wamekubaliana kuhabarisha Zaidi jamii kuhusu uhalisi wa mlipuko huo na kuwaondolea Imani potofu na uvumi kuhusu virusi vya ebola.

Maafisa hao walipeana habari kuhusu uzoefu wao tangu mlipuko huo ambapo wale wa DRC, walivutiwa matumizi ya jamii katika uhamasishaji nchini Uganda.

Licha ya kutosajiliwa kwa kisa chochote cha ebola Uganda tangu mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya DRC, imesalia chonjo na katika hatua zingine za hivi karibuni, wamechanja wahudumu wa afya wote walio msitari wa mbele kuzuia mlipuko huo kuenea hadi Uganda.

Ripoti zinasema watu zaidi ya mia mbili walioambukizwa virusi vya ebola tangu Agosti nchini DRC, wamethibitisha kuaga dunia.