Mifugo Sudan Kusini hatarini bila chanjo- FAO

23 Januari 2018

Nchini Sudan Kusini asilimia 30 ya mifugo iko hatarini kutokana na ukosefu wa chanjo dhidi ya magonjwa hatari, limesema shirika la chakula na kilimo duniani, FAO. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Nchini Sudan Kusini asilimia 30 ya mifugo iko hatarini kutokana na ukosefu wa chanjo dhidi ya magonjwa hatari, limesema shirika la chakula na kilimo duniani, FAO. Flora Nducha na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Flora Nducha)

Likisaka fedha kwa ajili ya kupatia chanjo takribani mifugo hiyo milioni 9, FAO imesema hadi sasa imepata asilimia 25 ya fedha inayohitajika kutekeleza kampeni hiyo.

Mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini Serge Tissot amesema kuhakikisha mifugo ina afya bora ni jambo muhimu kwa kuwa nusu ya wananchi wanategemea mifugo kwa ajili ya kukimu maisha yao.

Amesema wana haha kupata fedha hivi sasa kwa kuwa karibu mvua zinaanza na hivyo wakichelewa itakuwa vigumu kufika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kupatia Wanyama chanjo.

Hadi sasa wameshatoa chanjo dhidi ya magonjwa kama vile kimeta kwa wanyama 300,000 kwenye jimbo la Aweil, kaskazini-magharibi mwa Sudan Kusini.

Baadhi ya wafugaji ambao mifugo yao ilipatiwa chanjo wameshukuru wakisema awali walilazimika kutumia tiba za kienyeji kutibu mifugo yao kwa kuwa hawakuwa na dawa, na hivyo ng’ombe walidhoofika na walihofia kuwa wangalikufa.

FAO inasema iwapo itapata dola milioni 7.5 zilizosalia, itatumia siyo tu kwa chanjo bali pia kujenga vituo vitatu vya kuhifadhi chanjo hizo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter