Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kurejea kwa Warohingya Myanmar kuzingatie viwango vya kimataifa: UNHCR

Hamida, mwenye umri wa miaka 22 (kati) na mtoto wake Mohammed, mwenye umri wa mwaka moja, wanasubiri kupata msaada wa chakula pamoja na mamia ya wakimbizi wengine wa Rohingya katika kambi ya Wakimbizi ya Kutupalong, Bangladesh. © UNHCR / Andrew McConnell

Kurejea kwa Warohingya Myanmar kuzingatie viwango vya kimataifa: UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatambua ripoti kwamba serikali ya Bangladesh na Myanmar zimefikia muafaka wa kurejea Myanmar kwa wakimbizi wa Rohingya. John Kibego na taarifa kamili

(TAARIFA YA KIBEGO)

Kwa mujibu wa shirika hilo takribani wakimbizi 622,000 walifungasha virago na kukimbia jimbo la Kaskazini la Rakhine nchini Myanmar tangu Agosti 25 mwaka huu kutokana na wimbi la machafuko lililochochewa na kunyimwa uraia na miongo ya ubaguzi dhidi ya watu hao. Adrian Edward ni msemaji wa UNHCR Geneva.

(ADRIAN EDWARD CUT)

“UNHCR haijaona maelezo ya makubaliano hayo. Wakimbizi wana haki ya kurudi, na mfumo ambao utawawezesha kutimiza haki hii kulingana na viwango vya kimataifa, utakubaliwa. Kwanza kabisa, hii inamaanisha kwamba kurudi lazima kuwe ni kwa hiari, na kufanyike katika hali ya usalama na ya heshima ambayo itafungua nji ya suluhu ya kudumu.”

Ameongeza kuwa wakati huu hali katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar hairuhusu urejeaji salama na endelevu, watu bado wanakimbia na wengi wao wameathirika na ghasia, ubakaji, na maumivu ya kisaikolojia huku mgawanyiko mkubwa miongoni mwa jamii hauajapatiwa ufumbuzi.

Hivyo ameongeza kuwa UNHCR inatarajia kuona maelezo ya muafaka huo na iko tayari kusaidia serikali zote mbili katika kupata suluhu kuhusu zahma ya wakimbizi wa Rohingya Bangladesh , suluhu  ambayo inakidhi viwango vya kimataifa vya wakimbizi na haki za binadamu.