Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya choo India iende sambamba na huduma za maji na kujisafi

Haki ya choo India iende sambamba na huduma za maji na kujisafi

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za kupata maji safi na huduma za kujisafi amesema mtazamo wa haki za binadamu unahitajika katika kutokomeza vitendo vya watu kujisaidia hadharani nchini India.

Léo Heller ambaye leo kahitimisha ziara ya wiki mbili nchini humo amesema tamko lake linazingatia ukweli kwamba hivi sasa mkakati wa India wa ujenzi wa vyoo hauzingatii haki ya kibinadamu ya kuhakikisha watu wanapata maji safi na salama na huduma za kujisafi.

Amesema mkakati huo wa kuweka India iwe safi ulioanzishwa mwaka 2014 unataka watu kujengewa vyoo lakini wakati huo huo unakiuka haki za kupata maji na kujisafi kwa makabila madogo ambayo mengi yao huhusika na utapishaji wa vyoo.

Bwana Heller amesema hadi sasa hadi katika kipindi cha miaka mitatu India imejenga vyoo zaidi ya milioni 53 maeneo ya vijijini lakini hii haitoshelezi iwapo haiendi sambamba na mikakati ya kuelimisha watu kubadili tabia, kupatiwa maji ya kutosha na vyoo hivyo viwe vya gharama nafuu.

Ripoti yake ataiwasilisha mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwakani.