Hali ya kibinadamu CAR inazidi kuzorota - MINUSCA

9 Novemba 2017

Naibu mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika Kati, CAR Najat Rochdi leo katika mkutano na waandishi wa habari  kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani  ametoa tathamini ya hali ya kiusalama na kibinadam nchini humo.

Bi Rochdi  amesema hali ya kiusalama na hali ya kibinadamu CAR inazidi kuzorota kutokana migogoro ya wenyewe kwa wenyewe iliyoibuka tena  hivi karibuni  baina ya vikundi vilivyojihami na  vyombo vya usalama vya serikali.

(Sauti ya Najat)

"Hali ya kiusalama CAR inazidi kuzorota tangu mwezi wa tano mwaka huu kati ya  vikundi vya waasi vya makabila mbalimbali na vyombo vya usalama magharibi na kusini mashariki mwa nchi, hivyo husababisha ukimbizi wa ndani kwa raia tangu mwanzoni mwa mwaka huu . Hadi hivi sasa  idadi ya wakimbizi wa ndani imezidi laki 6 na  wengine laki 5    wamekimbilia nje ya nchi."

Kuhusu  mchango wa serikali ya CAR katika kuimarisha usalama na hali ya kibinadamu Bi. Rochdi amesema..

(Sauti ya Najat)

"Serikali ya CAR inakabiliwa na changamoto kubwa kiuchumi hivyo kushindwa kuwafikia wakimbizi hususani walioko mji mkuu Bangui [BON'GI] na Bambari. Upatikanaji wa huduma kwa wakimbizi hawa ni jambo jema sana kuweza kuokoa maisha yao.  Safari ya Katibu Mkuu Antonio Guterres huko CAR imekua ya manufaa kwa jamii ya CAR, kwani ilihamasisha mashirika ya kibinadamu kuweza kutoa misaada CAR."