Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umeme wasalia ndoto kwa wakazi wengi Afrika – Guterres

Umeme wasalia ndoto kwa wakazi wengi Afrika – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi serikali zichukue hatua kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya nishati salama iwe ya kupikia au ya kuangazia mwanga.

Bwana Guterres amesema hayo leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati akihutubia warsha kuhusu ushirikiano wa matumizi ya nishati duniani kwa lengo la kusongesha maendeleo endelevu.

Amesema hivi sasa watu bilioni moja duniani hawana kabisa huduma ya umeme ambapo milioni 500 wako Afrika na waliosalia wako ukanda wa Asia na Pasifiki.

Bwana Guterres amesema pamoja na kukosa umeme.

(Sauti ya Guterres)

“Watu bilioni 3 bado wanapika vyakula na kupatia joto nyumba zao bila kutumia nishati safi au teknolojia ambazo ni bora zaidi. Na zaidi  ya yote wengi wao wanaishi Afrika na Asia.”

Sambamba na uhaba wa nishati ya matumizi ya majumbani, Katibu Mkuu amesema uchafuzi wa hewa umevuka kiwango na kuwa chanzo cha watoto milioni 9 kufariki dunia kabla ya kuzaliwa mwaka 2015, asilimia 92 kati yao ikiwa ni nchi zinazoendelea.

Bwana Guterres ametaka nchi wanachama zizingatie mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris akisema bado kuna pengo kati ya ahadi zilizotolewa na utekelezaji.

image
Wajumbe kwenye kikao cha leo kuhusu ushirikiano katika kuzalisha nishati ili iweze kunufaisha kila mtu ulimwenguni. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
(Sauti ya Guterres)

 “Leo nasihi serikali na wadau wote duniani waongeze jitihada zao kubadili mfumo wa nishati duniani ili uwe wa maslahi kwa wote. Hebu na tuhakikishe kuwa ifikapo mwaka 2030 kila mtu bila kujali alipo, au anaishi umbali gani kutoka mjini, anapata huduma za nishati ya kisasa kwa gharama nafuu.”