Zaidi ya raia 500 wa Togo wanakimbilia Ghana- UNHCR

27 Oktoba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, linashirikiana na mamlaka nchini Ghana kuhusu uihifadhi wa raia wa Togo waliofika hivi karibuni nchini humo, wakikimbia machafuko ya kisiasa katika nchi yao.

UNHCR imesema hadi sasa, wamepokea wakimbizi 513 wengi wao wakiwa wanawake na watoto ambao wanasema wamekimbia ukiukwaji wa haki za binadamu baada ya maandamano ya kisiasa ya hivi karibuni.

Wakimbizi hao wamesema walitembea kutoka mkoa wa Mango huko Togo, na kutafuta hifadhi Ghana kupitia vijiji vya Chereponi, Zabzugu na Bunkprugu-Yunyou kaskazini magharibi mwa Ghana.

Serikali ya Ghana kupitia mamlaka husika kwa kushirikiana na UNHCR wanaendelea kutoa misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula , dawa na mahitaji mengine muhimu kwa wakimbizi hao. Barbar Baloch ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA BALOCH)

“Pia kuna taarifa ya kuwepo kwa wakimbizi wapya 30 wanaotafuta hifadhi kaskazini mwa Benin. Bado haijulikani kama hii inahusiana na hali ya sasa nchini Togo. Hivyo tunaendelea kuwasiliana mamlaka nchini Benin na Burkina Faso kuhusu misaada ya dharura kwa wakimbizi hao. “

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter