Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA pekee haiwezi leta amani CAR, bali mashauriano- Guterres

MINUSCA pekee haiwezi leta amani CAR, bali mashauriano- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehitimisha ziara yake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na kusema kuwa ingawa bado hali ni tete, mshikamano wa jumuiya ya kimataifa na nchi hiyo utaendelea.

Guterres amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu Bangui akisema kuwa hali ni tete kwa kuwa vikundi vilivyojihami vinachipuka kila uchao, raia, walinda amani na wafanyakazi wa misaada wanalengwa kila wakati huku mtu mmoja kati ya wanne akiwa ni mkimbizi wa ndani.

Amesema kama hiyo haitoshi, bado majimbo 14 kati ya 16 ya CAR hayako chini ya mamlaka ya ulinzi wa serikali huku ubakaji ukiendelea kutumika kila uchao kama silaha ya vita.

(Sauti ya Guterres)

 “Ni kweli kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati iko katika janga kubwa la kiusalama na kibinadamu. Lakini pia ni kweli kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ina taasisi za kidemokrasia na halali zinazoweza kusongesha nchi katika njia ya amani, usalama, utulivu na maendeleo.”

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (mwenye shati la buluu) akimsikiliza mkimbizi wa ndani alipotembelea kituo cha wakimbizi wa ndani cha "Site du Petit Seminaire St. Pierre Claver" kilichopo mjini Bangassou. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Bwana Guterres amesema ni kwa mantiki hiyo amesihi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liongeze idadi ya wanajeshi katika ujumbe wa kulinda amani wa umoja huo, CAR, MINUSCA.

(Sauti ya Guterres)

 “Kuchagiza mchakato wa kuimarisha na kusambaza jeshi la serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ushirikiano na MINUSCANinaamini kuwa ni vema kuwa na kikosi imara cha MINUSCA, lakini ni vyema pia kuwa na jeshi la kitaifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati.”

Amesema ingawa kuna watu wanataka MINUSCA itumie nguvu zaidi dhidi ya vikundi vilivyojihami bado walinda amani hao watatumua nguvu hiyo pale utulivu wa nchi utakapokuwa hatarini.

Amehitimisha kwa kuwakumbusha kuwa MINUSCA pekee haiwezi kuleta amani CAR bali amani italetwa kupitia mashauriano.