Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kiusalama nchini CAR bado si shwari-OCHA

Hali ya kiusalama nchini CAR bado si shwari-OCHA

Hali ya kiusalama nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR hususan maeneo ya Mashariki na Kusini-Mashariki mwa nchi inaendelea kuzorota na kusababisha idadi ya wakimbizi wa ndani kuongezeka na kufikia laki sita huku wakimbizi waliokuwa wamerejea nyumbani kutoka Cameroon wakilazimika kukimbia tena.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Cameroon ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu katika ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Najat Rochdi amesema hali ya kibinadamu inazidi kuzorota huku mahitaji yakiongezeka.

Aidha watoa misaada ya kibinadamu wamelazimika kusitisha shughuli zao kufuatia kuongezeka kwa ghasia.

Bi. Rochdi amesema kufuatia hali hiyo OCHA imelazimika kubadilisha namna inavyoendesha operesheni zake.

(Sauti ya Najat)

“Hatuwezi kuendelea na kufanya kazi kwa mazoea na kuwa na vituo kila mahali. Lakini kile ambacho tumefanya ni kuboresha baadhi ya vituo katika miji ambako hali ya usalama ni nafuu na kutoka hapo kupeleka misaada maalum kwa njia ya anga kwa sababu kwetu sisi kutowasilisha misaada na usaidizi wa kibinadamu kwa wanajamii sio mbadala.”