Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi warohingya wapatao 15000 wakwama mpakani mwa Bangladesh

Wakimbizi warohingya wapatao 15000 wakwama mpakani mwa Bangladesh

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeshtushwa na hali isiyoridisha ya kibinadamu kwa  maelfu ya wakimbizi wapya Rohingya waliokwama kwenye mpaka kati ya Bangladesh na Myanmar.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Andrej Mahecic amesema Jumapili usiku pekee waliingia wakimbizi kati ya 10,000 hadi 15,000 wakipitia mpaka wa Anjuman Para wilaya ya Ukhia kusini-mashariki mwa Bangladesh.

Bwana Mahecic amesema wakimbizi hao walikuwa wameamua kusalia Myanmar lakini walilazimika kukimbia baada ya vijiji vyao kuchomwa moto.

UNHCR na wadau wake wakiendelea kutoa misaada ya chakula na maji kwa wakimbizi wapya, wafanyakazi wengine wa shirika hilo pamoja na madaktari wasio na mipaka, MSF wanaendelea na kazi ya kubaini wanaohitaji matibabu.

AIdha Bwana Mahecic amesema UNHCR kwa kushirikiana na serikali ya Bangladesh bado wanaendelea na zoezi la kukamilisha kituo kipya cha mapokezi huko Kutupalong chenye uwezo wa kuhifadhi wakimbizi wapatao 1250, na pia kukamilisha shule kwa ajili ya watoto.

Takribani wakimbizi 582,000 kutoka Myanmar wameingia Bangladesh tangu vurugu dhidi ya warohingya zianze kwenye jimbo la Rakhine tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu.