Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utipwatipwa miongoni mwa watoto na barubaru unaongezeka:WHO

Utipwatipwa miongoni mwa watoto na barubaru unaongezeka:WHO

Idadi ya watoto na vijana barubaru wa kati ya umri wa miaka 5 hadi 19 walio na tatizo la utipwatipwa imeongezeka kote duniani katika miongo minne iliyopita, na endapo hali ya sasa itaendelea basi watoto na barubaru wengi watakuwa na utipwatipwa wa kupindukia au uzito mdogo kuliko kawaida imeonya leo ripoti mpya ya shirika la afya ulimwenguni WHO. Patrick Newman na tarifa kamili.

(TAARIFA YA PATRICK)

Ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la afya la Uingereza Lancet katika kuadhimisha siku ya utipwatipwa duniani inasema kiwango cha utipwatipwa kimeongezeka kutoka chini ya asilimia moja 1975 na kufikia karibu asilimia 6 kwa wasichana sawa na milioni 50 na asilimia 8 kwa wavulana sawa na milioni 74 mwa 2016.

Kwa ujumla utipwatipwa kati ya umri wa miaka 5-19 umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 10 duniani kutoka milioni 11 mwaka 1975 na kufikia milioni 124 2016.

Ili kukabiliana na tatizo hilo WHO imetoa mapendekezo sita ya kuzingatiwa kupambana na utipwatipwa ikiwemo  será za kudhibiti matangazo ya chakula na bei zinazochagiza hali hii. Fiona Bull ni meneja mipango, ufuatiliaji na uzuiaji wa maradhi yasiyo ya kuambukiza wa WHO.

(FIONA CUT)

“Masuala haya sita ni pamoja na kampeni kwa vyombo vya habari ili kumuelimisha kila mmoja athari na chanzo cha uzito wa kupindukia na utipwatipwa. Pili hatua za fedha na udhibiti kuweka mazingira mazuri na rahisi ya uchaguzi wa kiafya, kitu kingine ni mazingira ya shule kuhakikisha watoto wetu wana fursa ya chakula bora na mazoezi ya mwili, kuangalia vitu kama maeneo ya kujipumzisha, michezo na uwezekano na usalama wa wao kutembea na kuendesha baiskeli mara nyingi. Na hivi vitawasaidia watoto kujishughulisha zaidi na kuwasaidia kudhibiti uizito hivyo kuwa na afya njema.”

Ameongeza kuwa bila kudhibiti utipwatipwa kuna hatari kubwa ya watoto na vijana kutumbukia katika maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwemo ya moyo, kisukari, na saratani ambayo yana gharama kubwa kutibu kukiko kukinga.