Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yahitaji kufanya mengi kuhamasisha kanuni ya kupinga machafuko- Lajčák

UM yahitaji kufanya mengi kuhamasisha kanuni ya kupinga machafuko- Lajčák

Umoja wa Mataifa unahitaji kuchukua hatua zaidi ili kuchagiza kanuni ya kupinga machafuko ambayo inaambatana na maisha ya mwanaharakati wa haki wa India, hayati Mahatma Gandhi.

Hiyo ni kauli ya rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák wakati akihutubia hafla la kuadhimisha siku ya kupinga machafuko duniani leo Oktoba pili kwenye makao makuu ya Umoja huo, New York, Marekani.

Siku hii inaambatana na siku ya kuzaliwa kwa Mahatma Gandhi ambaye anatambulika kote duniani kama mwanzilishi wa kanuni ya kutumia mbinu ya amani ambapo Baraza Kuu katika azmio lake la kuanzisha siku hii linasisitiza kanuni ya kupinga machafuko na nia ya kuweka utamaduni wa amani, kuvumiliana na maelewano.

Bwana Lajčák amesema cha kusikitisha ni kwamba bado dunia ya leo haizingatii ndoto aliyokuwa nayo Mahatma Gandhi, huku watu wengi wakichagua ukatili ambapo kila siku kuna ushahidi wa uharibifu na madhila kwa binadamu, hali inayotokana na uchaguzi huo.

(Sauti ya Lajčák)

“Awali Mahatma Gandhi alikuwa ni mtu mmoja ambaye alifanya vitendo pekee yake, na vitendo hivyo vya mtu mmoja, vilichagiza wengine kufuata, na hii inatuonyesha tofauti halisi kati ya ukatili na amani. Mosi inahamasisha uoga, na nyingine inahamasisha hatua chanya. Kama kiongozi wa kupinga machafuko duniani, Umoja wa Mataifa unahitaji kufanya mengi ili kuchagiza kanuni hii na kuhamasisha wengine kuunga mkono.”