Urusi yabinya haki za binadamu huko Crimea- Ripoti

25 Septemba 2017

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeweka bayana vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwenye eneo la Crimea huko Ukraine ambalo linakaliwa na Urusi. Joseph Msami na ripoti kamili.

(Taarifa ya Msami)

Tangu mwezi Machi mwaka 2014, Urusi ilijitwalia eneo la Crimea nchini Ukraine na kulishikilia hadi hii leo, ambapo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema hadi sasa ukiukwaji wa haki za binadamu umepita kiasi.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, wataalamu wa haki za binadamu waliohusika na uchunguzi wametaja visa kama vile watu kukamatwa na kushikiliwa kiholela, watu kutoweshwa, mateso kwa waliokamatwa na kumetajwa kisa kimoja cha mauaji ya kiholela.

Na kama hiyo haitoshi Urusi imeweka sheria zake huku zile za Crimea zikiwekwa kando na hivyo kukosesha haki za msingi kama vile elimu.

Fiona Frazer ni mmoja wa wataalamu hao.

(Sauti ya Fiona)

“Kuanza kutumika kwa mfumo wa elimu wa kirusi umebinya haki ya watu wa asili nchini Ukraine kupata elimu katika lugha yao ya asili. Idadi ya wanafunzi wanaofundishwa kwa lugha ya Ukraine imepungua kwa kiasi kikubwa”

Ripoti imetoa mapendekezo kadhaa ikiwemo kwa serikali ya Urusi..

(Sauti ya Fiona)

“Kama mamlaka inayokalia eneo hilo, ina wajibu wa kimsingi wa kuhakikisha usimamizi wa haki, uwajibikaji na kupatiwa haki wale ambao haki zao zinakiukwa.”

Na pia kwa serikali ya Ukraine..

(Sauti ya Fiona) 

“Lazima itumie njia zote za kisheria na kidiplomasia ili kuendeleza na kuhakikisha haki za binadamu Crimea.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter