Usaidizi wa kibinadamu Sudan Kusini uende sambamba na maendeleo- Deng

23 Septemba 2017

Sudan Kusini imesema inaendelea kushirikiana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS ili kufanikisha kupelekwa kwa kikosi cha kikanda cha ulinzi wa amani, RPF.

Makamu Rais wa Sudan Kusini Taban Deng Dai amesema hayo akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo.

Amesema tayari kikundi tangulizi cha RPF kimewasili kwa lengo la kufanikisha masuala ya ulinzi wa amani kwa raia na hivyo kufanikisha makubaliano ya amani  yaliyofikiwa baina ya serikali na vikundi pinzani nchini humo

Kuhusu kuwezesha watoa huduma za kibinadamu kufika maeneo ya wahitaji, Bwana Deng Dai amesema serikali itahakikisha usalama wao huku akisema..

(Sauti ya Deng)

 “Wakati tunatambua kuwa kuokoa maisha ni jambo muhimu, tunapaswa pia kuimarisha fursa za kujikwamua kimaisha. Hatuwezi kuendelea kusafisha sakafu ilhali bomba liko wazi. Mifumo ya kizamani ya kwamba misaada ya kibinadamu ipatiwe kwanza kipaumbele halafu maendeleo yaje baadaye si sera inayofaa sasa kwa upande wa Sudan Kusini. Ni vyema kuhamasisha amani na utulivu kupitia mpango wenye mizania wa maendeleo na kufanya kazi.”

Amezungumzia pia suala la mizozano baina ya jamii, hali inayodhihirika kwenye vitendo vya uporaji wa mifugo, utekaji watoto na hata jamii kuwekeana kiwango kikubwa cha mahari.

Amesema kutokana na mazingira hayo serikali ya mpito  ya Umoja wa Kitaifa, TGONU kwa usaidizi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na wadau wengine …

image
Wakimbizi ambao wanarejea kwenye makazi yao huko Wau nchini Sudan Kusini baada ya amani kurejea. (Picha:UNMISS)

(Sauti ya Deng)“inawekeza katika kuboresha shughuli za kiuchumi baina ya jamii kama vile kujenga masoko, kukarabati shule, kujenga maeneo  ya kuhifadhi samaki na kutekeleza kwa amani upokonyaji silaha miongoni mwa jamii zilizojihami, mambo ambayo yameimarisha uhusiano baina ya jamii.”

Amesema ingawa kuna changamoto lakini kuna matumaini kwa kuwa kutokana na maendeleo hayo ya jamii ikiwemo wanawake na vijana kushiriki katika michakato ya amani..

(Sauti ya Deng)

“Hivi karibuni tumeshuhudia wakimbizi na wakimbizi wa ndani wakirejea kwa hiari kwenye vijiji vyao nah ii ni dalili ya utengamano na kuishi kwa amani”

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter