Zaidi ya watoto 850,000 hawana huduma za msingi Kasai DRC:UNICEF

15 Septemba 2017

Zaidi ya watoto 850,000 wameachwa bila huduma za msingi wakati huu machafuko baina ya makundi ya wanamgambo na vikosi vya serikali yakiendelea kwenye majimbo ya Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Joseph Msami na taarifa kamili

(TAARIFA YA MSAMI)

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF , watu takribani milioni 1.4 wametawanywa na machafuko hayo, huku zaidi ya laki tatu wakipata hifadhi katika nchi jirani ya Angola.

Watoto ndio wanaobeba gharama kubwa za machafuko hayo wakilazimika kupitia madhila kama kujeruhiwa, kuuawa, kuwekwa rumande na kuingizwa vitani na makundi ya wanamgambo huku ikielezwa kwamba karibu nusu ya wanamgambo hao ni watoto.

Luc mwenye umri wa miaka 12 ambaye jina limebadilishwa ili kumlinda, ametoroka kwenye kundi la wanamgambo alikokuwa askari anakumbuka ilivyokuwa alipoingizwa rasmi jeshini

(SAUTI YA LUC )

“siku ya ubatizo wangu nilizunguka na kuruka moto mara tatu, nilipewa vitu kumeza, baada ya hapo walichukua mapanga na kunichoma mara tatu kifuani, kisha wakanipa mifuko ya plastiki kumeza, wakisema kama ntakuwa makini kwa kitu fulani ninaweza kuwa askari. Baada ya hapo wakaniumiza kila mahali ili kuonyesha kwamba  hata kama nikishambuliwa ziwezi kuumia na mwishowe wakanipa kisu na gongo ili kwenda kwenye mapigano.”

Luc hivi sasa anapatiwa msaada na UNICEF ikiwemo chakula, mavazi, huduma zingine na ushauri nasaha na anatamani kurejea nyumbani kuwa na familia yake na kuweza kwenda  lakini haiwezekani kwa sasa kwa sababu ya unyanyapaa.

Wakati shule zimefunguliwa karibu kila sehemu duniani UNICEF inakadiria kwamba watoto 440,000 hawakumaliza muhula wa masomo mwaka jana kutokana na machafuko na usalama mdogo jimboni Kasai.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter