Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa viongozi kuchukua hatua nchini Sudan Kusini ni sasa

Wakati wa viongozi kuchukua hatua nchini Sudan Kusini ni sasa

Mzozo wa Sudan Kusini umeanzishwa na binadamu na viongozi nchini humo wana wajibu wa moja kwa moja kuutatua.

Hiyo ni kauli ya Naibu Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa El-Ghassim Wane aliyotoa wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani.

Kikao kilikutana  kujadili hali nchini Sudan Kusini ambapo Bwana El-Ghassim amewanyooshea kidole viongozi nchini humo akisema..

(Sauti ya EL Ghasim)

 “Hali mbaya ya kiuchumi na kuendelea kushuhudiwa kwa mzozo nchini humo kwa pamoja vimesababisha mazingira magumu kwa raia. Lakini viongozi hao hao wanaweza kuitoa nchi hiyo kutoka  kuzimu. Kile kinachohitajika ni azma ya kweli kisiasa kukomesha operesheni za kijeshi, na kufanya majadiliano ya amani na kufikia maelewano yanayohitajika kwa ajili ya amani nchini humo.”

Kwa upande wake mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan na Sudan Kusini Nicholas Haysom amesema wameainisha umuhimu wa kutofautisha malengo ya kila mkakati katika kusaka suluhu la amani akiongeza…

(Sauti ya Haysom)

“Juhudi za jukwaa la kuimarisha amani, mazungumzo ya kitaifa na mikakati mingine havipaswi kuchukua ajenda ya mkakati mwingine au kuwa na mashindano na nyingine.”

Naye mwenyekiti wa Tume ya pamoja ya uangalizi na tathimini, JMEC Festus Mogae amesema miaka miwili tangu kutiwa saini mkataba waamani ni hatua ndogo imepigwa hivyo..

(Sauti ya Mogae)

“Ni lazima tuongee kwa sauti moja na viongozi wa Sudan Kusini, na iendane na vitendo vyetu. Kunapaswa kuwa na uwajibishwaji wa wazi kwa vikundi visivyo na nguvu, wanaoharibu na wanaokiuka makubaliano.”

Hali nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kiuchumi, kisiasa na kiusaalma huku raia wakisaka hifadhi nchi jirani kila uchao.