Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa Kipindupindu Yemen wahatarisha zaidi wajawazito

Mlipuko wa Kipindupindu Yemen wahatarisha zaidi wajawazito

Nchini Yemen, kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu ni kubwa huku ikiripotiwa visa vipya 5000 kila siku.

Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA linasema zaidi ya wajawazito milioni moja wako hatarini zaidi na wanahitaji huduma ya dharura.

Miongoni mwao ni Ibsam ambaye anasema aliambukizwa Kipindupindu akiwa na ujauzito wa miezi 9 ambapo alipofika kituo cha afya hawakufahamu anasumbuliwa na nini hadi alipofikishwa hospitali iliyoko mji mkuu Sana’a ndipo alipatiwa matibabu.

Ili kukabili hali hiyo UNFPA sasa inasambaza siyo vifaa vya kujisafi bali pia vipeperushi kuhusu Kipindupindu na pia huduma za magari yanayopita kuelimisha jamii jinsi ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, zaidi ya visa 330,000 vya kipindupindu vimeripotiwa Yemen ambapo kati ya hivyo watu 1,800 wamefariki dunia.