Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaanza kugawa chakula kwa maelfu ya wakimbizi wa ndani DRC

WFP yaanza kugawa chakula kwa maelfu ya wakimbizi wa ndani DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP na washirika wake World Vision wamezindua operesheni ya dharura leo ya kugawa chakula kwa wakimbizi wa ndani 42,000 kwenye majimbo ya Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kwa mujibu wa WFP katika maeneo yanayofikika wanapanga kuwasaidia watu 25,000 Kasai ya Kati na 17,000 mkoa wa Kasai katika siku chache zijazo. Hata hivyo shirika hilo linasema linahitaji dola milioni 17.3 ili kuharakisha operesheni hiyo ambayo jumla inawalenga watu 250,000 wasiojiweza majimbo ya Kasai na Kasai Kati kuanzia Septemba hadi Desemba mwaka huu.

Mgao huo wa chakula umeanza katika mji wa Tshilumba na utaendelea mwezi wote huu. Kwa mujibu wa takwimu za WFP idadi ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula DRC imeongeza kutoka milioni 5.9 na kufikia milioni 7.7.