Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulio la kigaidi Burkina Faso

Guterres alaani shambulio la kigaidi Burkina Faso

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani shambulio la kigaidi lililotokea Jumapili kwenye mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou na kusababisha vifo vya watu 17.

Kupitia Naibu msemaji wake, Farhan Haq, ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Burkina Faso huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Na zaidi ya hapo msemaji huyo amenukuu akisema..

(Sauti ya Farhan)

“Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha ghasia hizo zisizochagua. Amesisitiza usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa Burkina Faso kwenye harakati zake za kukabiliana na misimamo mikali na ugaidi. Halikadhalika amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kushirikiana na kundi la nchi tano za ukanda wa Sahel zinapoimarisha jitihada za kukabiliana na changamoto lukuki za kiusalama ili kusongesha amani na maendeleo kwenye ukanda huo.”

Kundi hilo la nchi tano linajumuisha Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad.