Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mastercard na MediaCom zapiga chepuo harakati za WFP dhidi ya njaa

Mastercard na MediaCom zapiga chepuo harakati za WFP dhidi ya njaa

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limezindua kampeni iitwayo Kabiliana na Njaa kwa lengo la kuangazia mataifa manne yanayokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Taarifa ya WFP imesema uzinduzi huo uliofanyika Hispania, umetaja nchi hizo kuwa ni Sudan Kusini, Somalia, Nigeria na Yemen zikijumuisha zaidi ya watu milioni 20 walio hatarini kufariki dunia kutokana na njaa.

Kupitia kampeni hiyo kampuni za Mastercard na MediaCom huko Hispania zimetoa fursa za bure za matangazo kwenye maeneo mbalimbali ili kuangazia shida ya njaa kwenye mataifa hayo na hivyo kupata usaidizi.

WFP inasema njaa imesababisha watoto milioni 1.4 katika nchi hizo kukabiliwa na unyafuzi na kwamba hali ni mbaya zaidi kwa kuwa nchi hizo zinaingia kwenye kipindi cha mwambo ambapo mavuno yaliyopita yamekwisha na akiba ni kidogo.