Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji katika huduma za afya wahitajika kunusuru watoto Iraq

Uwekezaji katika huduma za afya wahitajika kunusuru watoto Iraq

Miongo ya vita na uwekezaji duni vimeweka shinikizo kubwa kwenye mfumo wa afya nchini Iraq. Hali hiyo imewafanya wanawake wajawazito na watoto kulipa gharama kubwa ya maisha yao limesema shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA, la afya WHO na la kuhudumia watoto UNICEF.

Mashirika hayo yanasema ingawa kuna hatua zilizopigwa katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito lakini imekuwa ni changamoto katika kupunguza vifo vya watoto hasa wa chini ya miaka mitano.

Watoto wachanga wako katika hatari zaidi kwa sababu ya mazingira mabaya wakati wa kujifungua , huduma hafifu za kuwapeleka hospitali kubwa, na huduma duni za uzazi hasa vijijini.

Mashirika hayo yameongeza kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama, huduma ya kulea kina mama, huduma ya kuwasaidia watoto wachanga wanaposhindwa kupumua wakizaliwa , huduma ya kangaroo kwa watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati au njiti, na kuzuia na kutibu maambukizi viitasaidia kuzuia vifo vya watoto wachanga.

Kwa kushirikiana na serikali mashirika hayo ymezindua mpango wa hatua ya kunusuru watoto wachanga (ENAP) ili kuwekeza katika kuboresha huduma za uzazi na watoto wachanga.