Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Venezuela lazima isitishe kuhukumu waandamanaji kijeshi na kuweka watu kizuizini

Venezuela lazima isitishe kuhukumu waandamanaji kijeshi na kuweka watu kizuizini

Serikali ya Venezuela ni lazima ikomeshe mfumo wa kuwakamata waandamanaji na ongezeko la matumizi ya mahakama za kijeshi kuwahukumu raia. Wito huo umetolewa leo na kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa .

Kundi hilo pia limeitaka serikali ya Venezuela kuheshimu haki za waandamanaji wote na mahabusu na kuwahakikishia usalama wao wa kimwili na kisaikolojia. Wataalamu hao wamesema wanatiwa hofu na madai ya watu kushikiliwa kiholela na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji pamoja na matumizi ya mahakama za kijeshi kwa raia.

Wameongeza kuwa vitendo hivyo vinakiuka waziwazi haki za watu za uhuru, na za kushitakiwa kwa haki mbele ya jaji asiye na upendeleo. Hali hiyo wamesema inakiuka haki ya uhuru wa watu kukusanyika kwa amani na kujieleza.