Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Kasai DRC wachukua mwelekeo wa kikabila:UM

Mgogoro wa Kasai DRC wachukua mwelekeo wa kikabila:UM

Machafuko katika majimbo ya Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC yanaonekana kuchukua mwelekeo wa kikabila imeonya ripoti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Taarifa kamili na John Kibego.

(Sauti ya Kibego)

Taarifa zilizokusanywa na timu ya uchunguzi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba baadhi ya ukiukwaji na ukatili uliotekelezwa katika majimbo ya Kasai unaweza kuwa uhalifu chini ya sheria za kimataifa.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo inatokana na mahojiano yaliyofanywa kwa watu 96 ambao wamekimbilia nchi jirani ya Angola kukimbia machafuko eneo la Kamonia Kasai. Timu ya Umoja wa Mataifa iliweza kuthibitisha kwamba kati ya Machi 12 na 19 Juni watu 251 walikuwa waathirika wa mauaji ya kulengwa na kutumia nguvu na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO umebaini makaburi ya pamoja 80 hadi sasa jimboni Kasai., Scott Campbell ni Mkuu wa Kitengo cha Afrika ya Magharibi na Kati, OHCHR..

(SAUTI YA .Scott)

"Manusura wamezungumzia kusikia mayowe ya watu wakichomwa moto wangali hai, wakiona wapendwa wao wakifukuzwa na kukatwa, wao wenyewe wakikimbia katika hofu kubwa. umwagaji damu huo ni wa kutisha zaidi kwasababu tumebaini ishara kwamba watu wanalengwa zaidi na zaidi kwa sababu ya makabila yao.”

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema ushahidi wao ni lazima uwe onyo kwa serikali ya DRC ili ichukue hatua sasa kuzuia machafuko ya aina hiyo kutosambaa zaidi na kuwa ni ya kusafisha kabila fulani.