Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya kipindupindu Yemen vinatarajiwa kuongezeka na kufika 600,000

Visa vya kipindupindu Yemen vinatarajiwa kuongezeka na kufika 600,000

Rais wa chama cha msalaba mwekundu ICRC,  Peter Maurer yuko katika ziara ya siku tano nchini Yemen wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliwa na viwango vya juu vya mlipuko wa kipindupindu huku idadi ya waathirika ikipanda kila siku.

Kwa mujibu wa ICRC idadi ya visa vya kipindupindu vinatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwisho wa mwaka 2017 na kufikia watu laki sita au mtu mmoja kati ya kila watu 45 nchini Yemen.

Bwana Maurer amesema cha kusikitisha zaidi ni kwamba mlipuko wa kipindupindu unaweza kuzuilika kwani ni janga lililosababishwa na binadamu kama moja ya athari za mzozo ambao umesambaratisha miundombinu na huduma za afya. Huku akisema, “Madhila ya watu wa Yemen yanatia hasira. Dunia iko katika usingizi na nchi hiyo inaelekea katika janga kubwa zaidi.”

Kusambaratika kwa mifereji ya majitaka na vituo vya kusafisha maji kwa dawa kumechangia katika kusambaa kwa ugonjwa.

Rais huyo atazuru Aden, Taiz na Sana’a ambako atajadiliana na maafisa kutoka pande mbili kwenye mzozo kuhusu hali ya kibindamu na jamii na kutoa wito kwa pande pinzani kuwezesha kufikiwa watu waliokwamba katika maeneo wanayoyadhibiti kutokana na  mzozo.