Ili kufikia SDGs ni lazimwa kuwekeza kwa wanawake- Amina Mohammed

Ili kufikia SDGs ni lazimwa kuwekeza kwa wanawake- Amina Mohammed

Haitowezekana kufikia malengo ya maendeleo endelevu bila kuwekeza kwa wanawake, amesema naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye anazuru Nigeria na pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Bi. Amina ambaye anaongoza ujumbe katika ziara hiyo ya aina yake ameandamana na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UNWomen, Mjumbe maalum kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo na mjumbe maalum wa muungano wa Afrika kuhusu wanawake, amani na usalama.

Akizungumza katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja naibu katibu mkuu huyo amesema wamekuwa na mikutano yenye ufanisi na kwamba ziara yao imejikita katika maswala muhimu ya amani, usalama na maendeleo, ikiwa na msisitizo kwenye haki za wanawake na uwezeshaji wao.

(Sauti ya Amina)

“Tunafahamu kuwa kuanzia kwa uchumi hadi utulivu na amani, hatuwezi kufikia malengo yetu iwapo tunawekeza katika nusu tu ya idadi ya watu. Nguvu kazi ni hazina muhimu kwa nchi na kwa bara zima, wanawake kwa kawaida ni nusu yake, lakini mara nyingi wanakosa uwekezaji unaohitajika.”

Bi Mohammed amesema kwamba utekelezaji wa maendeleo endelezu umekuwa na utata katika miaka ya hivi karibuni na licha ya kwamba malengo kama vile kumaliza umasikini uliokithiri na kuhakikisha elimu kwa wote ni muhimu, lakini mambo mengi yalihitaji kujumuishwa

(Sauti ya Amina)

“Mazingira tunamoishi ni yale ya vita na itikadi kali katika nchi nyingi na hususan Nigeria, kwa hiyo hapa tunachotaka kukufanya ni kuleta ujumbe wa wanawake: wanawake walioko katika nafasi za kufanya maamuzi; wanawake ambao hubeba mizigo wa majanga mengi tunayoshuhudia. Kuona ni vipi tutaibuka kutoka kwa hilo; ni vipi tunaweza kushirikiana katika kutafuta suluhu kwa ajili ya maendeleo endelevu.”

Ameongeza kwamba kusisitiza haki na mchango wa wanawake ni sehemu kubwa katika ukuaji wa kiuchumi.